
BAADA ya KMC kupoteza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo, anakabiliwa na presha kubwa ya kuondolewa katika benchi la ufundi la kikosi hicho licha ya matarajio makubwa aliyopewa tangu mwanzo.
Maximo aliyejiunga na KMC msimu huu, amekalia kuti kavu ndani ya kikosi hicho baada ya juzi kuchapwa bao 1-0 na Fountain Gate, ikiwa ni kichapo cha nne mfululizo kwa timu hiyo kati ya mechi tano za Ligi Kuu Bara ambazo ameiongoza.
KMC ilianza Ligi Kuu Bara vizuri kwa ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, kisha kuchapwa pia 1-0 na Singida Black Stars na Tanzania Prisons, ikalala 3-0 mbele ya Mbeya City, kisha kuambulia kichapo cha 1-0, kutoka kwa Fountain Gate.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo, Maximo amesema mwenendo wa kikosi hicho sio mzuri na hawana balansi nzuri katika maeneo yote mawili ya kujilinda na ushambuliaji, japo taratibu anaendelea kupambana na changamoto kubwa iliyopo.
“Ni hatua kwa hatua kwa sababu wachezaji ni wadogo na wanahitaji kuendelea kukuzwa zaidi katika vipaji vyao, sio suala la usiku mmoja kuona hilo likitokea, ila napata matumaini makubwa kutokana na kile wanachokionyesha,” amesema Maximo.
Hata hivyo, licha ya kauli hiyo ya Maximo, Mwanaspoti linatambua kocha huyo kwa sasa hayupo salama na kibarua chake, japo baadhi ya viongozi wanaamini ni mtu sahihi kutokana na kutambua vizuri kufundisha na kukuza soka hususani la vijana.
Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja tena Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kisha akaifundisha Yanga 2014, akiwa ni miongoni mwa makocha waliojizoelea umaarufu.
Maximo amerejea nchini akiwa na kumbukumbu nzuri, kwani ndiye kocha wa kwanza pia kuiongoza timu ya taifa ya Taifa Stars kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), iliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009.