KOCHA Mkuu wa Fountain Gate Princess, Noah Kanyanga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Oktoba 26, 2025 jijini Dodoma baada ya kuugua ghafla.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda ‘Mbuzi’ amesema Kanyanga alikuwa na changamoto ya kiafya muda mrefu iliyomsababishia kuugua ghafla na alipopelekwa hospitali usiku akafariki.

Mbuzi ameongeza kuwa taratibu za msiba leo Oktoba 26, 2025 watasafirisha kutoka Dodoma kuelekea Mburahati jijini Dar es Salaam na mambo ya mazishi watafahamu baada ya kufika.

“Jana jioni (Oktoba 25, 2025) alifanya mazoezi na timu na alionekana hana changamoto yoyote, saa 12 jioni hali ilibadilika na alipopelekwa hospitali hakuchukua muda akafariki,” amesema Mbuzi na kuongeza.

MSI 01

“Mambo yakikamilika mapema leo (Oktoba 26, 2025) tutasafirisha mwili kuupeleka Mburahati ambako ndio kuna ndugu zake, mambo mengine ya mazishi tutafahamu kwa familia.”

Kabla ya kuitumikia Fountain Gate, Kanyanga aliwahi kuzifundisha JKU Princess ya Zanzibar, Mburahati Queens, Gets Program, Ceasiaa Queens na JMK Youth Park.

Ni miongoni mwa makocha waliokuwa na mchango mkubwa kwenye soka la wanawake na ndiye alitoa nyota kadhaa waliokuwa tegemeo kwa Simba Queens, Yanga Princess na nyinginezo ikiwemo timu ya taifa.

Miongoni mwa nyota aliowafundisha ni Mshambuliaji wa zamani wa Simba Queens na Twiga Stars, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Maimuna Hamis ‘Mynaco’, Janeth Pangamwene na wengineo.

MSI 02

MIPANGO YAKE
Septemba 2025, Mwanaspoti ilifunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ilipokuwa kambi ya Fountain Gate Princess na ikafanikiwa kufanya mahojiano na kocha huyo.

Miongoni mwa mambo aliyofafanua kuyafanya msimu huu ni pamoja na kuirudisha Fountain Gate Princess ile yenye ushindani.

“Tumejipanga msimu huu, uliopita haukuwa mzuri kwetu kwani hatukumaliza kwenye nafasi nzuri, tumefanya usajili ambao tunaamini utakuwa na manufaa makubwa kwetu.

“Tunataka kushindana na vigogo Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess, tunaamini tunao uwezo wa kufanya hivyo tuna benchi la ufundi zuri, wachezaji na viongozi wenye uelewa wa soka hili,” hayo yalikuwa sehemu ya maneno ya Kanyanga katika mahojiano na Mwanaspoti enzi za uhai wake. 

MSI 03

WADAU WAMLILIA
Balozi wa Soka la Wanawake, Salva Mkindiko amesema Kanyanga alikuwa na matumaini makubwa msimu huu kwenye ligi ya wanawake.

“Hivi karibuni nimekuwa nikizungumza naye sana, ananiambia tunataka kuirudisha Fountain ile yenye ushindani, alikuwa na matamanio makubwa sana ila kiukweli nimeumia na sijaamini hadi nimzike.

“Juzi nimeongea naye kuna mchezaji alikuwa ananiambia, nashangaa napewa taarifa jana usiku alikuwa anaangalia mechi ya Yanga na Silver Strikers amefariki dunia, hakika tutamkumbuka, ni kocha alikuwa na maono makubwa sana,” amesema.

Elias Ilomo wa Singida Warriors, alikuwa chimbuko la mwanzo la soka la wanawake, amesema: “Dah, Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake. Kiufupi naweza kusema  Noah ndiye chimbuko la mwanzo kabisa la Singida Warriors kushiriki mashindano makubwa kwani mwaka 2018 wakati tunaanza kushiriki Ligi Daraja la Kwanza tulitumia wachezaji zaidi ya tisa kutoka JMK.

“Nakumbuka tulicheza mashindano yale tukiwa na mashabiki kutokea Dar es Salaam na ndio tulitengeneza msingi wa kutumia wachezaji chipukizi kwenye mashindano kwani wachezaji wote hao ilikuwa ndiyo mashindano yao ya kwanza makubwa ukitoa Umisseta na Umitashumta.”

Kiungo wa Yanga Princess, Mynaco amesema Kanyanga alikuwa kama mlezi wao na sio kocha pekee kutokana na kupambania malezi ya kila mchezaji akitamani wengi wao wafike mbali.

“Alikuwa na moyo wa kipekee sana, sisi bila yeye sidhani kama hata mpira tungecheza maana alitutengeneza Mburahati Queens tukawa wachezaji muhimu sana, Mungu ampe pumziko jema,” amesema Mynaco.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *