Madrid, Hispania. Real Madrid imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Barcelona katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania, LaLiga uliopigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Jijini Madrid.

Madrid leo imevunja unyonge baada ya msimu uliopita kuruhusu vipigo mara nne dhidi ya Wanacatalunya hao kutokea kaskazini, mashariki mwa Hispania.

Katika mchezo huo wa kibabe ilishuhudiwa Supastaa wa Madrid, Kylian Mbappé akiiandikia timu yake bao la kwanza katika dakika ya 22 akimalizia kwa ustadi mkubwa pasi ya Jude Bellingham.

Hata hivyo, bao la mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa halikuweza kudumu kwa Los Brancos baada ya mshambuliaji wa Barcelona, Fermin Lopez kusawazisha katika dakika ya 38 akifunga kwa msaada wa pasi ya Marcus Rashford.

Bellingham alihakikisha Madrid haiondoki kinyonge kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika baada ya kupachika bao la pili katika dakika ya 43 akimalizia kwa utulivu pasi iliyopigwa kichwa na Elder Militao.

Kipindi cha pili kilirejea timu zote zikionekana kushambuliana bila mafanikio ambapo mpaka dakika 90 za mwamuzi zinamalizika Madrid iliondoka kifuambele kwa ushindi wa mabao 2-1.

Ushindi ilioupata Los Blancos umekuwa wa kwanza tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho April 21, 2024 iliposhinda mabao 3-2 Santiago Bernabeu.

Madrid sasa imeipiku Barcelona kwa tofauti ya pointi tano kwenye msimamo wa LaLiga ikiongoza kwa jumla ya pointi 27 wakati Barcelona ikisalia ya pili ikiwa na pointi zake 22.

Katika dakika za majeruhi kwenye mchezo huo wa kukata na shoka Barcelona ilipata pigo baada ya kiungo wake Pedri kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje ya mchezo kwa kadi nyekundu.

Pedri hatakuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kitakacho ivaa Elche katika mechi inayofuata ya LaLiga itakayopigwa Novemba 2, 2025 kwenye Uwanja wa Olimpic Luis Company, Catalunya.

Katika mchezo wa leo Barcelona iliwakosa baadhi ya nyota wake muhimu kadhaa wakiwemo washambuliaji Robert Lewandowski na Raphina. Wengine ni viungo Dan Olmon a Gavi ambao wote wanauguza majeraha.

Pia yupo golikipa Marc Andre Ter Stegen pamoja na mabeki Andreas Christensen na Joan Garcia wakiwa majeruhi. Hata hivyo kocha Hans Frick naye hakuwa sehemu ya benchi la Barcelona akiitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye mechi dhidi ya Girona.

Kwa upande wa Madrid iliwakosa mabeki wake Antonio Rudiger na David Alaba ambao pia wanauguza majeraha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *