Dar es Salaam. Mwanachama  na  kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mama Jacqueline Malema Daniel, ametuma salamu za kheri na pongezi kwa wagombea wote wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa Tanzania  uliopangwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, akisisitiza umuhimu wa amani, umoja na utiifu kwa mamlaka katika kipindi cha kampeni na upigaji kura.

Kupitia salamu zake, Mama Malema ameeleza kufurahishwa na uteuzi wa  Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais kupitia CCM, pamoja na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, akisema uteuzi huo ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo wanachama na Watanzania kwa ujumla katika uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nachukua nafasi hii kuwatakia ushindi wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge, hadi udiwani. Ujumbe wangu kwa wanachama wenzangu ni kwamba, twende tukatiki ni mitano tena.

Tuheshimu mamlaka na tusiwachokoze,” amesema Mama Malema.

Amesema kuwa uchaguzi ni kipindi cha kuonesha umoja, nidhamu na ustaarabu, huku akiwataka wanachama wa CCM kudumisha amani na kuonesha mfano wa demokrasia ya kweli.

Amefafanua kuwa ushindi wa chama hicho hautokani na maneno, bali unajengwa kupitia kazi, upendo na mshikamano wa wanachama wake katika kila eneo la nchi.

“Mama yetu, Rais Samia, tuko pamoja na wewe. Una mitano tena. Tunaamini katika uongozi wako wa hekima, uadilifu na upendo kwa Watanzania wote,” amesisitiza Mama Malema.

Mama Malema amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta matumaini makubwa kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, uimarishaji wa huduma za jamii, na jitihada za kuinua uchumi wa nchi.

Amesema mafanikio hayo ndiyo msingi wa imani inayompa nguvu CCM kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza kwa miaka mingine mitano.

Aidha, ametoa wito kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana katika ngazi zote.

“Ni jukumu letu kuhakikisha tunalinda heshima ya chama chetu na kuendeleza misingi ya waasisi wetu,” ameongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *