Dar es Salaam. Wazalishaji wa sukari nchini wamesema sekta hiyo imeingia katika kipindi cha ustawi mkubwa, kutokana na ongezeko la uzalishaji kwa asilimia 54, huku ikitazamiwa kuwa uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu utafikia tani 350,000 katika nusu ya pili ya msimu wa 2025/26.

Kiwango kinachotarajiwa kutosheleza soko la ndani na kuimarisha ushindani wa kikanda.

Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA), kimetabiri upatikanaji wa sukari kufikia angalau tani 350,000 katika nusu ya pili ya msimu wa uzalishaji wa 2025/26 kiwango ambacho kinatarajiwa kuzidi mahitaji ya ndani na kusaidia kudhibiti bei sokoni.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen leo Jumapili Oktoba 26, 2025, Katibu Mtendaji wa TSPA,  Kennedy Rwehumbiza, alisema jumla ya wazalishaji saba wakubwa TPC Moshi, Kagera Sugar Limited, Mtibwa Sugar Estate, Kilombero Sugar Company, Bagamoyo Sugar Limited, Manyara Sugar Company, na Mkulanzi Holding Company tayari wamezalisha zaidi ya tani 340,000 za sukari hadi sasa.

“Kiwango hiki ni sawa na asilimia 147 ya mahitaji ya ndani ambayo yanakadiriwa kuwa takriban tani 230,000. Ukilinganisha na kipindi kama hicho msimu uliopita, hii ni ongezeko la asilimia 54, likionesha uimara wa sekta na ufanisi wa uzalishaji,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa bei sokoni, ambapo kilo moja ya sukari sasa inauzwa kati ya Sh2,600 na Sh3,000.

“Asilimia 80 ya sukari yote inauzwa ndani ya nchi, jambo linalowanufaisha watumiaji kwa upatikanaji wa uhakika na bei stahimilivu. Hii ni matokeo ya uratibu mzuri katika mnyororo mzima wa thamani na dhamira ya wazalishaji kujibu mahitaji ya soko,” ameongeza.

Katika masoko ya kikanda, sekta ya sukari inaendelea kufanya vizuri. Kufikia katikati ya Oktoba 2025, Tanzania ilikuwa imeuza nje takriban tonne 85,000 za sukari, na kupata mapato ya zaidi ya dola milioni 72 za Marekani kutokana na mauzo hayo.

Wazalishaji wanasema mauzo hayo yanaonyesha ushindani unaoongezeka na mwelekeo wa sekta hiyo katika kusaidia ajenda ya viwanda nchini, na kuiweka sukari kama bidhaa muhimu ya kiuchumi, si chakula tu bali pia chanzo cha mapato ya fedha za kigeni.

Masoko lengwa ya mauzo hayo ni pamoja na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda, miongoni mwa mengine.

Mwanzo mwa mwezi huu wakati wa kampeni za Uraisi mkoani Kagera Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia  Suluhu Hassan katika kuboresha sekt ya uzalishaji wa sukari nchini.

Bashe ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, serikali imefanikisha mapinduzi makubwa katika sekta ya sukari.

“Maamuzi yaliyofanywa na Serikali mwaka mmoja uliopita yamewezesha sekta ya sukari kuhudumia Watanzania kwa ufanisi. Leo sukari haizidi Sh2,800 kwa kilo, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo bei ilikuwa juu zaidi,” alisema Bashe.

Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Prof Kenneth Bengesi, pia alishasema kwamba uzalishaji wa ndani sasa umepita mahitaji ya kitaifa.

“Hali ilivyo sasa, isipokuwa kutokee dharura, hatuna tena haja ya kuagiza sukari kutoka nje. Uzalishaji wetu unatosheleza mahitaji ya ndani kikamilifu,” alisema.

Taarifa za TSPA zinaonyesha kuwa Kampuni ya Sukari Kilombero inaendelea na mradi wa upanuzi wa K4, ambao utakamilika ukiwa umeongeza uwezo wa uzalishaji kwa tonne 144,000 kwa mwaka. Baada ya kukamilika, uzalishaji wa jumla wa Kilombero utazidi tonne 270,000.

Wakati huo huo, Kagera Sugar Limited inapanua shughuli zake kupitia uwekezaji mkubwa katika kilimo cha miwa na maboresho ya teknolojia za uzalishaji, ikilenga kuongeza maradufu uzalishaji wake wa sasa wa tonne 140,000 kufikia msimu wa 2029/30.

Rwehumbiza alisema mwenendo wa upanuzi huo umevutia mtaji mpya, huku sekta hiyo ikishuhudia kuingia kwa wazalishaji wapya wanne Golden Sugar, Lake Agro, Mufindi Paper, na Eagle-Agrotechikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji na mazingira mazuri ya udhibiti wa sekta.

“Kuingia kwa wawekezaji wapya ni kielelezo cha kuimarika kwa sera za serikali zinazolenga kukuza kilimo-biashara endelevu na chenye ushindani,” amesema Rwehumbiza.

Zaidi ya uzalishaji wa sukari ghafi, sekta inapanuka katika bidhaa zenye thamani ya juu, ikiwemo usafishaji wa sukari, uzalishaji wa ethanoli na Extra Neutral Alcohol (ENA). Hatua hizi zinaendana na mkakati wa TSPA wa kujenga mnyororo wa thamani endelevu, unaoleta faida kubwa na kuchangia katika uchumi wa kijani wa Tanzania.

TSPA imesisitiza kwamba mafanikio ya sekta hayawezi kupatikana bila ushirikiano thabiti kati ya wazalishaji, serikali, na wakulima wadogo wanaolima miwa. Mageuzi katika mifumo ya malipo, uimarishaji wa teknolojia za kidijitali, na huduma za ugani yamehakikisha wakulima wanapata malipo kwa wakati na kwa haki, hivyo kuwezesha viwanda kufanya kazi kwa ufanisi wa juu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *