Shinyanga. Moto uliozuka saa tatu usiku wa Oktoba 25, 2025 katika mtaa wa Igalilimi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga umeteketeza vibanda sita vya biashara huku saba vikiokolewa pamoja na samani zake.

Kaimu Kamanda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Fatma Sato amesema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme katika moja ya vibanda vinavyouza vifaa vya umeme.

Amebainisha kuwa katika moto huo  hakuna madhara kwa binadamu ikiwemo majeruhi au vifo.
Amesema moto huo ulisambaa kwa kasi kutokana na kuwepo kwa mlundikano wa mizigo katika eneo hilo yakiwamo magodoro.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia athari za moto ulioteketeza vibanda sita vya biashara usiku wa kuamkia leo Oktoba 26,2025 katika mtaa wa Igalilimi Manispaa ya Kahama. Picha na Amina Mbwambo

Fatuma amesema jeshi hilo limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu utoaji wa taarifa za majanga ya moto mapema.

Amesema, “Maduka yaliyoungua katika eneo hili ni sita pamoja na samani zake, tumefanikiwa kuokoa vibanda saba na samani zake, hakuna madhara yoyote kwa binadamu ikiwemo vifo na majeruhi” amesema na kuongeza:

“Tunashauri wananchi kujitahidi kutoa taarifa za moto mapema ili kuwahi eneo la tukio, na tunawashauri wafanyabiashara kuweka vifaa vya awali vya kung’amua moshi ili kuweza kubaini moto katika hatua za awali uweze kudhibitiwa.”

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amesema wanaendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo wakati wote ambapo Serikali inaendelea na taratibu za kulirejesha katika hali ya kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita aliyefika kukagua madhara ya moto huo amesema, Serikali inaendelea na jitihada za kurejesha eneo hilo katika hali yake ya kawaida kwa kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na mmiliki wa eneo hilo.

Amesema tathmini ya hasara ya mali inaendelea, na kuwakumbusha wananchi na wafanyabiashara kuchukua hatua za mapema kudhibiti majanga yanayozuilika ili kuepusha hasara ya mali na mitaji yao.

Amesema, “Haya majanga yanazuilika ni tofauti na majanga mengine kama kimbunga, mvua hivyo chukueni hatua za mapema kuweka ving’amuzi vya moto, fanyeni ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo yenu na muepuke kujiunganishia umeme kienyeji.”

Wananchi waliojitokeza kushuhudia moto uliozuka usiku wa kuamkia leo Oktoba 26,2025 katika mtaa wa Igalilimi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Siyajali Kabika mkazi wa Kahama amesema, “moto uliwaka wakati maduka yakiwa yamefungwa, tumesaidiana na zimamoto kuokoa baadhi ya vitu na tunashukuru mgodi wa Buzwagi uliongeza nguvu ya gari ya kuzimia moto ndipo ukadhibitiwa.”

Naye Paulo Hamka mmiliki wa kibanda cha biashara katika eneo hilo amesema alipata taarifa akiwa nyumbani saa tatu usiku ndipo alipowahi eneo la tukio na kuanza jitihada za kuuzima moto.

Amesema, “Ninaiomba serikali ya wilaya kuboresha vifaa ikiwemo gari la zimamoto liwe na maji ya kutosha wakati wote, na wajitahidi kuwahi eneo la tukio.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *