
Unguja. Ofisi ya Mufti Zanzibar, imeeleza sababu za kutofunga madrasa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu ili kuondosha hofu na kujenga taharuki kwa wananchi kwamba hakuna amani.
Pia, imewatahadharisha waandishi wa habari kuzingatia weledi na kuacha kuandika habari zitakazoleta taharuki na kusababisha mgawanyiko miongoni mwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumapili Oktoba 26, 2025, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema hawakuona sababu ya kufunga madrasa Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi kwa sababu kufanya hivyo ni kuleta wasiwasi na taharuki kwa wananchi.
“Hatukufunga kwa sababu bado kuna amani, sasa tukifunga madrasa kwa sababu ya uchaguzi tunaongeza taharuki na kuonesha kana kwamba hakuna amani, bado tuna amani hali ni shwari,” amesema katibu mtendaji huyo.
Sheikh Mfaume amesema kuna taarifa potofu zinazushwa mitandaoni baada ya taarifa kutolewa za kufungwa kwa shule.
Amesema; “ kufungwa kwa shule kuna sababu. Baadhi zitatumika kama vituo vya kupigia kura na si vinginevyo, sisi madrasa zetu hazitumiki kama vituo vya kupigia kura, kwa nini tuzifunge? Hivyo natamka kwamba madrasa hazitafungwa, tunaendelea na madarasa yetu kama kawaida.”
Sheikh Mfaume amesema ofisi ya Mufti inasisitiza kuendeleza amani na utulivu wakati wa uchaguzi kwa kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine, ofisi ya Mufti imewatahadharisha waandishi wa habari kutotoa taarifa za taharuki ambazo hazina ukweli kuelekea Oktoba 29, 2025, siku ambayo Watanzania watapiga kura kuwachagua viongozi wao watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Divisheni ya Fatwa na Utatuzi wa Migogoro, Sheikh Shaaban Al Batashi amesema taarifa za upotoshaji zinasababisha hofu, wasiwasi na kuleta mgawanyiko miongoni mwa wanajamii.
“Taarifa hizi zinaathiri mtazamo wa wananchi na kuunda mitazamo isiyo sahihi na kutengeneza chuki,” amesema.
Pia, amesema katika kutoa taarifa za upendeleo na kumbeba mtu fulani zinaweza kuchochea chuki miongoni mwa wagombea na wafuasi wao na kuwavunja moyo wananchi wakaacha kujitokeza kwenda kupiga kura, na baadaye kufanya shughuli zao za kijamii ikiwamo kujitafutia mahitaji yao ya kila siku.
Naye Mwalimu wa Dini, Masjid Rahman Mombasa, Sheikh Masoud Ahmada amesema ni wajibu kuchuja mambo badala ya kuandika kila kitu.
“Ukiandika uongo unasababisha uovu, ukweli ndio utakuweka huru na kuokoa katika hatari, ni vyema kuchukua tahadhari na kuwa wakweli,” amesema.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana amewaondolea hofu wananchi kwamba hakutakuwa na changamoto ya usalama hivyo wasifunge biashara zao kisa uchaguzi.