Rombo. Mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Adolf Mkenda ameahidi kuwa endapo ataaminiwa tena na wananchi kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, atahakikisha kituo cha forodha cha Tarakea kinafanya kazi saa 24 ili kurahisisha biashara za mpakani na kukuza uchumi wa eneo hilo.

Akizungumza leo Jumapili, Oktoba 26, 2025, katika Tarafa ya Mashati, Profesa Mkenda amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara wa mpakani kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kuongeza mapato na kuchochea maendeleo ya jimbo na taifa kwa ujumla.

“Niwaombe wananchi wa Rombo, ifikapo Oktoba 29 mjitokeze kwa wingi kupiga kura. Nina matumaini makubwa na jimbo hili. Pale kituo cha forodha cha Tarakea tutahakikisha biashara zinafanyika saa 24,” amesema Profesa Mkenda.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wengi wa Rombo wamekuwa wakikumbana na changamoto wanapofanya biashara na nchi jirani ya Kenya, kutokana na upande wa Tanzania kutokuwa wazi kwa saa 24, tofauti na upande wa Kenya ambao unafanya kazi muda wote.

“Wapo Warombo wengi wanaofanya biashara Kenya, lakini wanapata ugumu kwa sababu upande wetu haufanyi kazi saa 24. Wenzetu wa Kenya tayari wanafanya hivyo, nasi tunapaswa kwenda sambamba nao,” ameongeza.

Kuhusu soko la Holili, Profesa Mkenda alisema atalifanyia maboresho makubwa ili liwe soko la kimataifa litakalouza matunda, mboga mboga na nafaka katika nchi jirani na hata zile za Mashariki ya Kati, ikiwemo Dubai.

Katika sekta ya kilimo, Profesa Mkenda ameahidi kuweka kipaumbele kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ili kuongeza tija, hasa katika kilimo cha ndizi ambacho ndicho tegemeo kuu la wakulima wa Rombo.

“Mashamba yetu ni madogo, lakini yanaweza kutoa mazao mengi endapo tutatumia teknolojia za kisasa za umwagiliaji. Hili tutalifanya kuwa kipaumbele chetu,” amesema.

Aidha, ameahidi kusimamia ujenzi wa masoko ya kisasa katika maeneo ya Mrere na Usseri ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora zaidi.

“Tutashirikiana na Halmashauri pamoja na Tamisemi kuhakikisha tunaongeza masoko yaliyopangwa vizuri katika maeneo hayo,” amesema Profesa Mkenda.

Vilevile, aliwahimiza wananchi wa Rombo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura, wakichagua CCM ili kukamilisha miradi na ahadi zilizotolewa.

“Tunashukuru kwa mwamko mkubwa mliouonyesha katika kampeni. Tunaomba mjitokeze kwa wingi kumpigia kura Rais wetu Samia Suluhu Hassan aendelee kuongoza nchi, na mimi niendelee kuwatumikia kama Mbunge wenu,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Katangara Mrere (CCM), Venance Mallel, amewahimiza wananchi wa kata hiyo kujitokeza siku ya uchaguzi na kukichagua chama hicho, akiahidi kushirikiana na Mbunge huyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Endapo tutachaguliwa, tutaendelea kushirikiana na viongozi wetu kuhakikisha tunatekeleza ahadi zote tulizozitoa kwa wananchi,” amesema Mallel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *