
Katavi. Wananchi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wanatarajia kunufaika na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (Tactic).
Mradi huo utagharimu Sh21.9 bilioni na utatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Hayo yameelezwa leo Jumapili, Oktoba 26, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miundombinu kupitia mradi huo.
Amesema hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kwa kuboresha miundombinu ya usafiri, mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya halmashauri.
Amemtaka Mkandarasi M/s Chongqing International Construction Corporation (CICO) kuhakikisha kazi inafanyika kwa ubora, kasi na kukamilika kwa wakati, huku akiwataka watendaji wa Manispaa ya Mpanda na Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) kushirikiana katika usimamizi wa mradi huo.
Kupitia mkataba huo, CICO itajenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 8.4, jengo la usimamizi wa mradi na ununuzi wa magari manne ya kufuatilia utekelezaji wa kazi.
Mradi unatarajiwa kuanza rasmi Novemba Mosi mwaka huu na kukamilika ndani ya miezi 15.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Tactic kutoka Tarura, Emmanuel Manyanga amesema lengo la mradi ni kuboresha miundombinu ya miji 45 nchini na kuzijengea uwezo halmashauri katika usimamizi wa maendeleo ya miji na ukusanyaji mapato.
Amesema mpango huo unaolenga kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji, utaiwezesha Manispaa ya Mpanda kuvutia wawekezaji, kupanua shughuli za kiuchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.
“Tunataka kuona miji yetu ikitoa huduma bora na yenye tija kwa wananchi. Huu ni mwanzo wa mageuzi makubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi,” amesema Manyanga.