Simba imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa sare isiyo ya mabao na Nsingizini Hotspurs.
Licha ya sare hiyo, Simba imefuzu kwenda hatua ya mbele baada ya ushindi mzuri wa mabao 3-0 ugenini, ukitosha kuwatupa nje Nsingizini ambao ilikuja na akili mpya mbele ya wenyeji wao.
Hatua ya Simba kufuzu imekamilisha idadi ya timu nne za Tanzania, kutinga makundi ikitangulia na Yanga ambao wako mashindano hayo huku Singida Black Stars na Azam nazo zikienda hatua kama hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kipindi cha kwanza kilikuwa na mvutano mkubwa katikati ya uwanja kuliko eneo la mwisho la umaliziaji kwa timu zote kupambana kumiliki mpira huku washambuliaji wakikosa utulivu.
Shambulizi zuri lilikuwa dakika ya 27 ambapo Nsingizini walitengeneza lakini kipa Yakub Seleman aliruka imara na kupangua shuti lilopigwa.
Shambulizi hilo ndio pekee lililotengeneza shuti lililolenga lango kwenye dakika 45 za kwanza, ingawa Simba ndio iliyomiliki mpira vizuri kwenye kipindi hicho cha kwanza kushinda wapinzani wao.
Hali hiyo ya timu zote kushambuliana kwa zamu iliendelea kipindi cha pili ambapo Simba ndio walikuwa wa kwanza kutengeneza shambulizi zuri dakika ya 55 kupitia Elie Mpanzu lakini kipa Dlamini Thabo alisimama imara na kupangua.
Mabadiliko matano
Simba ilifanya mabadiliko matano dakika ya 57 wakiwatoa Morrice Abraham, Elie Mpanzu, Jean Charles Ahoua na Yusuf Kagoma nafasi zao zikichukuliwa na Alassane Kante, Neo Maema, Steven Mukwala na Jonathan Sowah.
Mabadiliko hayo yalikwenda kuiimarisha Simba eneo la kiungo cha ukabaji na kile cha kushambulia huku pia ikiifanya Simba kucheza na washambuliaji wawili mbele.
Nsingizini ilifanya shambulizi lingine zuri dakika ya 64 kupitia mpira wa adhabu ndogo shuti la Joel Madondo likagonga mwamba na kurudi uwanjani.
Mpaka mwisho wa mchezo timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana huku wekundu hao wakinufaika na ushindi wa mabao 3-0 mchezo wa kwanza na kutinga makundi.
Yakub Seleman, David Kameta,Antony Mligo, Rushine de Reuck, Chamou Karaboue, Yusuf Kagoma/Allasane Kante,Joshua Mutale/Aweso Aweso, Morice Abraham/Steven Mukwala,Kibu Denis, Jean Charles Ahoua/Neo Maema, Elie Mpanzu/Jonathan Sowah.
Nsingizini Hotspurs
Dlamini Thabo,Adeleke, Ade,Vuyo Macina/Ayanda Gadlela,Kwakhe Thwala, Kingsley Kwakyi, Dlamini Senzo, Mavuso Thubelihle/Sambulo Simelane,Khumalo Sizwe/Veemak Jordyn, Shongwe Nkosingphile, Joel Madondo/Mthethwa Mvuselelo, Dlamini Sinenkosi.