Dar es Salaam

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), imewataka watumishi wote wa umma walioko katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Imesisitiza kuwa ushiriki wa watumishi wa umma ni sehemu muhimu ya kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na amani ya nchi — nguzo kuu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu unaokadiriwa kufikia $1 trilioni ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, jijini Dar es Salaam, Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, amesema watumishi wa umma wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha dira ya maendeleo ya Taifa inatimia, kwa kuwa wao ndio watendaji wakuu wa sera na mipango ya Serikalii.

“Ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi ni zaidi ya kutekeleza haki ya kikatiba. Ni tendo la kizalendo linaloimarisha misingi ya utawala bora na kuonesha dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi na uchumi imara,” amesema Mauki.

Ameongeeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka dira thabiti ya maendeleo inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi unaotegemea uwazi, uadilifu na ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Mauki, kupiga kura ni wajibu wa kiraia unaoimarisha umoja, uthabiti wa Taifa na uwajibikaji.

Aidha, Mauki amebainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi.

Kupitia jukumu hilo, OMH imeendelea kuhimiza ustawi wa rasilimaliwatu, uwajibikaji wa viongozi na utendaji bora wa taasisi za umma kama sehemu ya msingi wa kujenga uchumi imara na endelevu.

#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *