
Dar es Salaam. Katika dunia ambayo mara nyingi imekuwa ikiwatenga watu wenye ulemavu. Bahati Female Band, bendi ya wanawake inayojumuisha watu wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu, imeanzisha mradi wenye jina la ‘Nithamini’, unaolenga kuleta mabadiliko chanya katika mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu katika sanaa.
Akizungumza katika Listening Party ya Nithamini Ep, yenye jumla ya nyimbo tano Sote ni sawa, Nithamini, Mwanamke na Africa. Irene Lugakingila, msanii na Mratibu wa Bahati Female Band amesema wazo la ‘Nithamini’ lilitokana na changamoto ambazo wanakutana nazo wasanii wenye ulemavu katika kazi zao za kila siku.
“Haki za walemavu kwenye sanaa hazichukuliwi kiukubwa na pia miundombinu yao siyo salama kwenye ufanyaji wao wa kazi. Kwa hiyo hii Nithamini au Bahati Female Band ni sehemu tunaongelea na kuweka chachu kwa kujenga miundombinu ambayo ni salama kwa watu wenye ulemavu
“Wito wetu kwa Watanzania watushike mikono katika hii mikoa ambayo tunaenda. Tumetengeneze nyimbo tuungane kwa pamoja hata na serikali kupitia hii project kwa sababu tutaenda mikoa mitano,”amesema Irene
Aidha kwa upande wake Pili Maguzo, Mkurugenzi wa Bahati Female Band amesema bendi hiyo ilianza na watu sita lakini kwa sasa wamefika 30
“ Mradi huu umetoka moyoni ni kilio cha walemavu kutaka kuthaminiwa kama binadamu wengine na wasanii. Kupitia muziki, tunapaza sauti kupinga unyanyapaa na dharau ambazo watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana nazo kwa muda mrefu. Kuna wakati tunafika kwenye shoo lakini watu wanadhani tumeenda kuomba misaada,”amesema
Mbali na hayo akizungumza katika mjadala ulioandaliwa katika uzinduzi wa mradi huo, Hassan Tuli, Afisa Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alieleza sanaa ni nyenzo yenye nguvu kubwa katika kutetea haki za watu wenye ulemavu.
“Sanaa hugusa hisia moja kwa moja. Wimbo au uchoraji unaweza kubadilisha fikra za jamii kwa haraka zaidi kuliko hotuba. Tatizo ni kwamba bado hakuna mikakati ya kitaifa inayowapa nafasi wasanii wenye ulemavu katika majukwaa makubwa,” alisema Tuli.
Akaongeza kuwa, miundombinu duni katika kumbi za maonyesho, studio na maeneo ya sanaa inawanyima watu wenye ulemavu fursa ya kuonyesha vipaji vyao.
“Hata kwenye matamasha ya kitaifa, hawapewi nafasi. Inasikitisha kuona wasanii wengi wenye ulemavu wakijiimbia wao wenyewe kwa sababu hawajumuishwi,” aliongeza.
Pamoja na jitihada hizo, familia bado zinatajwa kuwa na nafasi kubwa katika kufanikisha ndoto za wasanii wenye ulemavu.
Latifa Abdallah, mwanamuziki na dansa wa bendi hiyo, anasema baadhi ya familia huogopa kuwekeza kwa hofu ya gharama au mtazamo wa jamii.
“Familia inapaswa kumtazama mtoto mwenye ulemavu kama sehemu ya uwekezaji. Wazazi wengi wanakata tamaa mapema, lakini kipaji kinapozimwa, ndoto ya mtoto nayo inakufa,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dk Herbert Makoye amesema hapo awali taasisi hiyo haikuwa inawachukua vijana wenye ulemavu katika programu zao, lakini hali imeanza kubadilika.
“Taasisi wakati inaanza ilikuwa ina shida kwa sababu walikuwa hawachukui vijana wenye ulemavu. Lakini kwa kutambua vijana wote wakiwemo wenye vipaji lazima wapewe nafasi sawa, kwa sasa suala la ubaguzi limeondoshwa. Taasisi inapokea vijana wote na tunajitahidi hata miundombinu kuirekebisha ili iwe rafiki. Nia ni kwamba tufikie sehemu ambayo kila anayefika pale ajisikie vizuri,” amesema