Wawakilishi wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati katika Fainali za Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake mwaka huu, JKT Queens wamepangwa kundi B la mashindano hayo ambayo yatafanyika mwezi ujao huko Misri.
Kundi hilo la JKT Queens linakutanisha timu nne ambazo kila moja imewahi kushiriki mashindano hayo hapo nyuma kwa nyakati tofauti.
Bingwa mtetezi wa mashindano hayo, TP Mazembe ni miongoni mwa timu nne zinazounda kundi hilo, ikiingia kwa lengo la kutetea taji lake huku ikiwakilisha kanda ya Soka ya Afrika ya Kati.
Wawakilishi wa Kanda ya Soka ya Kusini mwa Afrika (COSAFA), Gaborone United ambayo ilishiriki Fainali hizo za Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake kwa mara ya kwanza mwaka jana, inarejea tena katika fainali za mwaka huu na kutakuwepo pia na Asec Mimosas ya Ivory Coast inayowakilisha kanda ya Afrika Magharibi (WAFU).
Katika droo ya mashindano hayo iliyochezeshwa leo, timu zilizopangwa katika kundi A la mashindano hayo ni FC Masar (Misri), AS FAR (Morocco), 15 de Agosto (Guinea Ikweta) na US FAS Bamako (Mali).
Ni timu mbili tu katika Fainali hizo mwaka huu ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ambazo ni 15 de Agosto na US FAS Bamako.
Fainali za Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake zitafanyika Misri kuanzia Novemba 8 hadi Novemba 21 mwaka huu.
Bingwa wa mashindano hayo atavuna kiasi cha Dola 600,000 (Sh1.5 bilioni) na mshindi wa pili ataondoka na kitita cha Dola 400,000 (Sh987 milioni).
JKT Queens haikuwahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi katika fainali hizo.