,

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Huku kukiwa hakuna mgombea maarufu wa upinzani aliyeidhinishwa kushiriki katika uchaguzi wa Jumatano, 29/10/2025, Watanzania wengi wanahisi kura hiyo si mashindano bali ni kama kutawazwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akikabiliwa na uchaguzi wake wa kwanza wa urais.

Samia mwenye umri wa miaka 65 amekuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya kifo cha rais John Magufuli mwaka 2021. Alisifiwa kwa upande mmoja kwa dhamira yake ya kukomesha ufisadi lakini alikosolewa kwa ukandamizaji wake wa kimabavu juu ya upinzani na mtazamo wa kutatanisha dhidi ya janga la Covid.

Rais Samia, ambaye alikuwa makamu wa rais, alionekana kama pumzi ya hewa safi – na kwa mtindo wake wa kirafiki, alianzisha mageuzi ambayo yalionekana kuwa mabadiliko makubwa kutoka kwa sera za mtangulizi wake.

Sera yake yenye ‘R nne’ – “reconciliation, resilience, reform and rebuilding” yaani “maridhiano, uthabiti, mageuzi na kujenga upya” – ilifungua tena Tanzania kwa wawekezaji wa kigeni, kukarejesha uhusiano wa wafadhili na kuvutia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

“Alifanya mabadiliko, uhusiano uliopotea kati ya Tanzania na mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia ulirejeshwa,” mchambuzi wa kisiasa Mohammed Issa aliiambia BBC.

Lakini katika kipindi cha miaka miwili hivi iliyopita, nafasi ya kisiasa imepungua kwa kiasi kikubwa – na kulengwa kwa wakosoaji wa serikali na sauti za upinzani kunasemekana kuwa katika hali mbaya zaidi sasa kuliko ilivyokuwa chini ya Magufuli, huku utekaji nyara na mauaji ya mara kwa mara sasa yakiripotiwa.

“Samia aliingia kwa sauti ya maridhiano, lakini sasa amekuwa amekuwa mwenye kufanya maamuzi magumu ambayo wengi hawakutarajia kutoka kwake,” alisema Bw Issa.

“Sasa analaumiwa pakubwa kwa baadhi ya mambo kama vile utekaji nyara, mauaji, ukandamizaji wa upinzani na masuala mengine kuhusu usalama.”

Hii imeakisiwa katika ripoti za Freedom House, shirika la utetezi wa demokrasia na haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani, ambalo liliiweka Tanzania kama taifa “huru kwa kiasi fulani” mwaka 2020 na “lisilo huru” mwaka jana.

Serikali haijazungumzia tuhuma hizo.

.

CCM ya Samia imeshinda kila chaguzi tangu kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa mwaka 1992, lakini kampeni huwa na mijadala mikali kati ya vyama pinzani.

Wakati tume ya uchaguzi ikiwa imewaachia wagombea urais 17 kugombea urais wakati huu, chama kikuu cha upinzani Chadema kimezuiwa huku kiongozi wake Tundu Lissu akikabiliwa na kesi ya uhaini.

Alikuwa akitoa wito wa mageuzi ya uchaguzi kabla ya kukamatwa kwake mnamo mwezi Aprili – na chama sasa kinawataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo.

Makamu wake, John Heche, naye alikamatwa wiki iliyopita – na aliiambia BBC kabla tu ya kuwekwa kizuizini kwamba kile kinachoitwa mageuzi ya Rais Samia ni mambo yasio na msingi: “Ndiyo, mikutano ya hadhara iliruhusiwa tena, lakini leo Chadema haiwezi kutekeleza wajibu wake kwa sababu ahadi zilikuwa za uongo.”

Wakati huo huo, mgombea urais Luhana Mpina, kutoka chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani, ACT Wazalendo, pia ameenguliwa – mara mbili.

Alifaulu kurejeshewa ugombeaji wake na Mahakama Kuu baada ya kuzuiliwa kutokana na suala la kiutaratibu – lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipokata rufaa mwezi uliopita, tume ya uchaguzi iliamua kuunga mkono upande wake.

Hii inaviacha vyama vidogo vya upinzani kama vile CHAUMMA na CUF kwenye kinyang’anyiro hicho, lakini kiuhalisia hakuna nafasi ya kumzuia Samia kushinda wadhifa wake wa sasa.

“Udhibiti wa chama tawala, kutengwa kwa upinzani na upendeleo wa kitaasisi kunadhoofisha uaminifu wa uchaguzi. Fursa finyu ya ushiriki wa umma na uhamasishaji mdogo wa wapiga kura hudhoofisha ushirikishwaji wote,” alisema mchambuzi wa kisiasa Nicodemus Minde katika ripoti ya hivi majuzi ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS).

Hii imewaacha baadhi ya wapiga kura, kama mkazi wa Dar es Salaam, Godfrey Lusana, kukata tamaa.

“Hatuna uchaguzi bila upinzani thabiti. Mfumo wa uchaguzi hauko huru. Tayari tunajua nani atashinda. Siwezi kupoteza muda wangu kupiga kura,” aliambia BBC. “Kama tume ya uchaguzi ingekuwa huru kweli, ningepiga kura.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *