SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetangaza kwamba, kwa timu zote zilizofuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, zina uhakika wa kupewa Dola za Marekani 700,000 (Sh1.7 bilioni za Tanzania).

Hiyo inamaanisha kwamba, Yanga na Simba zina uhakika wa kuvuna kiasi hicho cha fedha kikiwa ni kikubwa zaidi ya upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam na Singida Black Stars zilizofuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika, zenyewe kila moja ina uhakika wa kuingiza Dola za Marekani 400,000 (Sh995.5 milioni za Tanzania).

Ukiweka kando fedha hizo za CAF, kumekuwa na hamasa inayotolewa kwa timu za Tanzania zinapopata ushindi ambapo kila bao thamani yake ni Sh5 milioni.

Katika mechi nne hadi zinafuzu makundi, Azam ndiyo imevuna fedha nyingi kutokana na kushinda zote kwa idadi kubwa ya mabao ambayo ni 13. Kwa idadi hiyo ya mabao, Azam imepata Sh65 milioni kupitia hamasa hiyo ya Bao la Mama.

Inayofuatia ni Yanga iliyovuna Sh35 milioni katika mechi tatu ilizoshinda ikipoteza moja, kisha Singida Black Stars (Sh30 milioni) nayo imeshinda mechi tatu ikiwa na sare moja, mwisho ni Simba (Sh20 milioni) imeshinda mechi mbili zote ugenini na sare mbili ilizopata nyumbani.

Msimu huu imeshuhudiwa Tanzania kwa mara ya kwanza ikipeleka timu nne hatua ya makundi katika michuano ya CAF ambazo ni Yanga na Simba (Ligi ya Mabingwa), Azam na Singida BS (Kombe la Shirikisho).

Kwa kufika hatua ya makundi, rekodi zinaonesha Simba hii ni mara ya saba katika kipindi cha miaka nane ambapo mbili ilikuwa upande wa Kombe la Shirikisho (2021-2022 na 2024-2025) huku Ligi ya Mabingwa ni (2018-2019, 2020-2021, 2022-2023, 2023-2024 na sasa 2025-2026).

Yanga kuanzia 2016 hadi sasa, imecheza makundi mara sita, tatu Kombe la Shirikisho (2016, 2018 na 2022-2023) na tatu Ligi ya Mabingwa ikiwa mfululizo (2023-2024, 2024-2025 na sasa 2025-2026).

Azam ilijaribu mara 10 bila ya mafanikio kabla ya 11 ambayo ni msimu huu kufuzu makundi Kombe la Shirikisho.

Azam iliyoanza kushiriki michuano ya CAF mwaka 2013, ilikuwa haijawahi kucheza makundi ambapo mara mbili imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na 2024-2025, zote imeishia hatua ya awali.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya msimu huu kufuzu makundi, huko nyuma imewahi kujitahidi na kufika hatua ya pili.

Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2013 na kuishia hatua ya kwanza, kisha 2014 (hatua ya awali), 2016 (hatua ya pili), 2017 (hatua ya kwanza), 2019–2020 (hatua ya kwanza), 2021–2022 (hatua ya pili), 2022-2023 (hatua ya pili), 2023-2024 (hatua ya kwanza).

Singida Black Stars imeifikia rekodi ya Namungo ya msimu wa 2020–2021 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi licha ya kwamba haikuendelea zaidi ya hapo ikimaliza mkiani bila pointi.

Timu za Tanzania ambazo zimeshiriki michuano hiyo mbali na Simba na Yanga ni KMC (2019–2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021–2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025), ambazo hazikutoboa. Ilikuwepo na Azam iliyowahi kushiriki mara nane kabla ya msimu huu kuvunja mwiko.

Kwa Singida Black Stars, mtihani ilionao ni kufuzu hatua ya robo fainali na kuweka rekodi mpya ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza kutoka Tanzania na kufika mbali zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *