
Kuna sehemu fulani nchini Sudan ambapo ukifika unaweza kusahau kwamba kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea.
Wanawake waliovalia mavanzi yenye rangi angavu na viatu vya plastiki, katika milima ya Jebel Marra nchini huondoka kila asubuhi na watoto wao juu punda, watoto wakiwa wamebebwa, kutunza mashamba.
Katika hali ya hewa kama ya Mediterania na kwa kutumia udongo wenye rutuba, wanapanda karanga, machungwa, tufaha na stroberi, mazao adimu kwa nchi ambayo sasa inakabiliwa na moja ya migogoro mibaya zaidi ya njaa duniani. Kabla ya mzozo huo, machungwa ya kikaboni ya Jebel Marra yalithaminiwa sana kote nchini kwa utamu wake.
Eneo la milimani katika sehemu hii ya magharibi mwa Darfur limejaa vilele vya kijani kibichi, haswa sasa kwani ni msimu wa mvua.
Sudan iliyobaki iko karibu na janga.
Kote nchini, kutokana na mapigano ya miaka miwili na nusu ambayo yamelemaza kilimo, karibu watu milioni 25, nusu ya idadi ya watu, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, wakiwemo zaidi ya 600,000 ambao wanakabiliwa na njaa, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Lakini katika nyanda za juu za Jebel Marra, tatizo si kulima chakula, ni kutoa mazao.
“Karibu tunayauza bure na wakati mwingine tunayaondoa njiani [kwenda sokoni], kwa sababu yanaoza,” anasema Hafiz Ali, muuzaji wa machungwa katika mji wa Golo, ambao uko katikati ya milima katika jimbo la kati la Darfur.
Kutokuwa na usalama na hali mbaya ya barabara hufanya usafiri kuwa mgumu sana.
Chanzo cha picha, Zeinab Mohammed Salih
Jebel Marra ni eneo la mwisho lililobaki linalodhibitiwa na Jeshi la Ukombozi la Sudan, Abdulwahid (SLA-AW). Kundi hili lenye silaha limebaki bila kuegemea upande wowote katika vita vya sasa. Halijawahi kusaini makubaliano ya amani na mamlaka huko Khartoum kuanzia mwaka 2003 na mzozo kuhusu Darfur wakati huo.
SLA-AW imedhibiti kile ambacho wenyeji wanakielezea kama “maeneo yaliyokombolewa” kwa zaidi ya miongo miwili.
Sasa, likiwa limezungukwa na vita pande zote, eneo hilo linazidi kutengwa.
Upande wa magharibi na kaskazini, Vikosi vya wapiganaji wa RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu wamefunga barabara kuu. Upande wa kusini, maeneo ya RSF hulipuliwa karibu kila wiki na jeshi la Sudan, mashambulizi haya pia yanagharimu maisha ya raia.
RSF pia inadhibiti maeneo upande wa mashariki.
Matokeo yake ni mazingira yaliyofungwa ambapo wakulima na wapatanishi hawawezi tena kufikia masoko ya kitaifa katika miji ya el-Fasher iliyo umbali wa kilomita 130 (maili 82), au Tine, kwenye mpaka wa Chad, umbali wa kilomita 275 (maili 170).
Kuna njia mbadala nyingine lakini hakuna hata moja iliyo na ufikiaji sawa wa kitaifa na zote zinahusisha safari za hatari.
Tawila, iliyo pembezoni mwa eneo la SLA-AW, imekuwa eneo la soko la muda. Iko kwenye barabara ya kuelekea el-Fasher, ambayo imekatishwa na kuzingirwa na RSF, na imekuwa makazi ya makumi ya maelfu ambao wameweza kukimbia mji huo.
Kwa sababu ya ugumu wa kuhamisha mazao zaidi, kuna usambazaji kupita kiasi sokoni na matokeo yake bei hapa zimeshuka.
Kuna baadhi hapa wanaotafuta kununua vifaa ili kujaribu kusafirisha mazao kwenda el-Fasher, biashara hatari sana na inayohatarisha maisha.
Kupata bidhaa hadi hapa kumekuwa changamoto kila wakati na chakula wakati mwingine kinaweza kuoza njiani.
“Kusafiri kama kilomita 12, inakuchukua siku nzima ya kuendesha gari milimani na kwenye matope,” anasema Yousif, muuzaji wa matunda huko Tawila. Lakini sasa, anasema, ukosefu wa usalama unafanya mambo kuwa mabaya zaidi.
Katika Darfur ya Kati, makubaliano ya hivi karibuni kati ya viongozi kutoka kabila la Fur, linalotawala hapa na wahamaji wa Kiarabu yameruhusu biashara ndogo katika baadhi ya maeneo.
Masoko yamefunguliwa tena katika mji wa Nertiti unaodhibitiwa na SLA-AW, ambapo wanawake wa Kiarabu huuza maziwa ya siki na wakulima wa Fur huleta matunda na mboga.
“Soko hufunguliwa mara moja tu kwa wiki. Usafiri bado ni hatari,” anasema mfanyabiashara kutoka Nertiti.
“Ujambazi wa kutumia silaha bado unatokea barabarani, hata baada ya makubaliano.”
Matunda na mazao sasa yanaweza kuuzwa sokoni katika Zalingei inayodhibitiwa na RSF, mji mkuu wa jimbo la Darfur ya Kati. Lakini wanamgambo wa Kiarabu wanaoshirikiana na RSF mara nyingi wanashutumiwa kwa kuwanyanyasa au kuwashambulia raia katika eneo hilo, ingawa makundi hayo yanakana shutuma hizo.
Kila Alhamisi, ambayo ni siku ya soko, idadi ya vituo vya ukaguzi kati ya Nertiti na Zalingei huongezeka, wakati mwingine hufikia zaidi ya dazeni mbili. Lakini kadiri magari mengi yanavyokuwa barabarani siku za soko, watu wengi zaidi hutumia fursa hiyo kusafiri.
Vituo vya ukaguzi, baadhi vikiwa na wapiganaji wa RSF na vingine na wanamgambo wa Kiarabu, wakati mwingine husimamiwa na mtu mmoja tu mwenye silaha aliyevaa nguo za kawaida, ambaye anadai ada. Madereva mara nyingi hujaribu kujadiliana huku abiria wakiendelea kutazama kimyakimya.
Chanzo cha picha, Zeinab Mohammed Salih
Kurudi katika eneo la Jebel Marra, vituo vya ukaguzi vya SLA-AW hulinda kila barabara inayoingia milimani, na wanaume wenye silaha pia hudai pesa.
Mifuko hupekuliwa kwa magendo, hata ikiwa ni pamoja na krimu za kuchubua ngozi, zinazotumika sana kwingineko nchini Sudan, huchukuliwa.
Wakati wa kuingia katika eneo linalodhibitiwa na SLA-AW, licha ya amani ya kiasi, kuna dalili wazi za mzozo kwingineko nchini.
Malori yaliyojaa watu wanaokimbia mapigano, hasa karibu na el-Fasher, yanaweza kuonekana kila siku.
Wengi wao hupata hifadhi katika shule, kliniki na maeneo mengine ya umma wakipokea msaada mdogo wa kibinadamu, mashirika ya misaada yanajitahidi kupita katika vituo vyote vya ukaguzi.
Huko Golo, mji mkuu wa eneo la SLA-AW, mwanamke ambaye alikuwa ametoroka kutoka el-Fasher, alielezea hali mbaya. Sasa anajificha darasani na familia nyingine 25 zilizowasili hivi karibuni.
“Hatuna kipato. Hakuna kazi za kufanya, nilikuwa nikifanya kazi kama nesi na naweza kulima, lakini ardhi hapa ni ya watu wanaojifanyia kazi wenyewe tu. Hatujui la kufanya,” mwanamke huyo alisema.
Alipokuwa akizungumza, wagonjwa, wazee walilala chini na watoto walikuwa wakipiga kelele kwa njaa. Angalau kutakuwa na utulivu kwani chakula ambacho hakingeweza kuchukuliwa kutoka Golo kitapatikana.
Hili ni eneo la Jebel Marra, ulimwengu wa ajabu uliozungukwa na vita. Ulimwengu wa milima ya kijani kibichi na maporomoko ya maji. Ulimwengu wa matunda angavu na yenye sharobati.
Mfanyabiashara mmoja wa matunda alisema amepoteza matumaini katika pande zote mbili zinazopigana.
“Sisi si sehemu ya vita, tunataka tu kuuza machungwa yetu.”