MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Isimani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), William Lukuvi, amesema ujenzi wa barabara ya Iringa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa kilomita 104, utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Tarafa ya Idodi na maeneo jirani.
Akifunga kampeni za uchaguzi katika jimbo hilo, Lukuvi amesema barabara hiyo imekuwa kilio cha muda mrefu, hasa vipindi vya mvua ambapo usafiri umekuwa wa tabu na kusababisha wakulima kupata hasara kwenye mazao yao kutokana na kuchelewa kuyafikisha sokoni.
“Serikali ya Awamu ya Sita imetekeleza kwa vitendo ahadi yake. Kukamilika kwa barabara hii kutafungua fursa za utalii, kuongeza ajira na kuwezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi,” alisema Lukuvi.
Amesema ujenzi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni 142 unaonesha dhamira ya serikali kuboresha miundombinu kwenye maeneo yote nchini bila kuacha nyuma vijiji vilivyo mbali na miji.
Baadhi ya Wananchi wa Idodi wamesema ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha usafiri na kuongeza mapato kupitia vivutio vya utalii vilivyopo katika eneo hilo ikiwemo Hifadhiya Taifa ya Ruaha .
“Tumeteseka kwa miaka mingi, hasa kipindi cha masika. Sasa mazao yetu yatafika sokoni kwa wakati na Ruaha italeta wageni wengi,” alisema mmoja wa wananchi.
Wameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo ni nguzo muhimu ya kubadilisha maisha yao na kuongeza fursa za uwekezaji katika biashara, hoteli na usafirishaji.
Mradi huu unatarajiwa kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Jimbo la Isimani na kuiwezesha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuwa miongoni mwa maeneo yanayochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kupitia utalii.
#StarTv update
