
Baraza la katiba la Cameroon limemtangaza Rais aliyeko madarakani Paul Biya kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa karibu asilimia 54% ya kura.
Matokeo rasmi yanaonyesha kuwa, Biya alipata asilimia 53.66 ya kura, huku mpinzani wake mkuu na mshirika wake wa zamani, Issa Tchiroma Bakary, akipata asilimia 35.19.
“Mgombea Biya Paul ametangazwa kuwa Rais wa Jamhuri, baada ya kupata wingi wa kura halali zilizopigwa,” alisema Clement Atangana, Rais wa Baraza la Katiba.
Ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 57.76, huku asilimia 42.24 wakijiondoa katika mchakato wa kupiga kura.
Hata hivyo, matokeo haya yanapingana na madai ya mgombea wa upinzani Issa Tchiroma, ambaye kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Madai hayo yamechochea hasira na maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo hadi sasa watu wasiopungua watano wameripotiwa kuuawa.
Maandamano yamezuka huko Douala, mji mkuu wa kiuchumi wa Cameroon, kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Rais mteule Paul Biya bado hajawahutubia wananchi wa Cameroon baada ya kuchaguliwa tena Jumatatu, lakini chama tawala kimepongeza ushindi wake “chini ya ishara ya ukuu na matumaini” katika machapisho ya mtandaoni.
Hakujawa na maoni yoyote kutoka kwa serikali kuhusu ripoti kwamba watu wenye silaha wamefyatua risasi na kuua watu wawili karibu na nyumba ya mshindi wa pili Issa Tchiroma Bakary.
Akiwa yuko madarakani kwa takribani miaka 43, Paul Biya (92) sasa ataongoza kwa muhula wa nane wa miaka mingine saba.lea kubaki madarakani.
Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.