Chanzo cha picha, EATV
Oktoba 29, 2025, ni siku muhimu kwa Tanzania. Ni siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani tukio la kikatiba linalotazamwa kama kilele cha demokrasia ya taifa.
Lakini mwaka huu, siku hiyo hiyo imechukua sura mbili. Wakati serikali na vyama vya siasa vinawahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura, makundi mengine yanayojitambulisha kama wanaharakati yanahamasisha maandamano, wakisema ni njia ya kupaza sauti zao dhidi ya kile wanachokiona kama kukwama kwa mageuzi ya kisiasa.
Wito huu wa pande mbili umeibua mjadala mpana kuhusu namna Watanzania wanavyotafsiri demokrasia yao. Kwa upande mmoja, wapo wanaoamini ushiriki katika uchaguzi ni njia bora ya kuleta mabadiliko ndani ya mfumo uliopo.
Kwa upande mwingine, wapo wanaoona mfumo huo huo umekuwa kikwazo cha mageuzi, hivyo kuamua kuutumia uchaguzi huo huo kama jukwaa la kutoa ujumbe wa kutoridhika kwao.
Jeshi la Polisi nalo linasisitiza maandamano yanayopangwa yanaashiria kuleta vurugu na yanavunja sheria. “Atakayevunja sheria Oktoba 29 asilaumu”, anasema Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime.
Migongano ya haki mbili za kikatiba
Kwa mujibu wa Ibara ya 20 ya katiba, na hata sheria ya vyama vya siasa, watu wana haki ya kukusanyika pamoja na kutoa maoni au mawazo yao kwa umma ikiwemo kufanya maandamano baada ya kutoa taarifa kwa mkuu wa polisi katika eneo husika ambapo maandamano yatafanyika.
Je, wanaotaka kuandamana sasa wametoa taarifa? Hakuna aliyeweka wazi kuhusu hilo. Si Polisi wala wanaotaka kuandamana, hatua inayozidi kuleta sintofahamu na kuendelea kujenga mvutano.
Hii itakuwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi urejee mwaka 1995, Tanzania kukabiliwa na mvutano wa wazi kuhusu namna ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia, unaohusisha haki hizi mbili kwa wakati mmoja.
Upande mmoja unasisitiza kuwa kupiga kura ni haki na wajibu wa kikatiba unaojenga taifa. Upande mwingine unadai haki hiyo hiyo ya kikatiba kuandamana kwa amani kama njia mbadala ya kutoa ujumbe kwa serikali.
Mfuatiliaji wa siasa za Afrika Mashariki, Simon Kulwa (si jina lake halisi), anasema hali imefika hapa kwa sababu “kambi mbili zimeshindwa kusikilizana.”
“Wanaotaka kuandamana wanaona mfumo wa sasa wa kisiasa hauna haki wala uwazi. Kwao, ni bora kupaza sauti kuliko kushiriki katika mchakato wanaoamini hauna usawa. Wanaosisitiza kupiga kura wanawaona waandamanaji kama wanaotaka kuvuruga amani,” amesema.
Mzizi wa hali hii, kwa mujibu wa wachambuzi, ni hoja ya muda mrefu, ambayo ni mabadiliko ya kisiasa na kikatiba.
Makundi yanayoitisha maandamano yamekuwa yakisisitiza kupatikana kwa Katiba mpya, mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na uhuru wa kisiasa.
Vuguvugu hili lilianza baada ya kauli ya “No Election, No Reforms” (Hakuna Uchaguzi bila Mageuzi) kuibuliwa na chama cha upinzani CHADEMA.
Hata hivyo, chama hicho hakijawahi kutangaza rasmi kushiriki maandamano ya Oktoba 29. Wengi wanaona mwamko huu umechukua sura ya kiwanaharakati zaidi kuliko kichama, ukiendeshwa kwa nguvu kubwa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii.
Chanzo cha picha, HabariLeo
Serikali inasema madai ya “ukosefu wa mageuzi” si ya kweli. Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, serikali imefanya maboresho 15 ya sheria za uchaguzi mwaka 2024 ili kuimarisha uwazi na uadilifu wa uchaguzi.
“Kwa mara ya kwanza Tanzania imepata sheria mahsusi ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ya mwaka 2024, hatua muhimu ya kuimarisha uwajibikaji,” alisema Ndumbaro.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na kuzuia wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, kuondoa utaratibu wa wagombea kupita bila kupingwa, kuwaruhusu wafungwa kupiga kura, na kuweka masharti kwa wasimamizi wa uchaguzi kutokuwa wanasiasa waliowahi kushiriki siasa katika miaka mitano iliyopita.
Lakini kwa wapinzani wa serikali, mageuzi hayo ni ‘kiini mcho’. Wanasema hayagusi matatizo ya msingi kama uhuru wa kweli wa Tume ya uchaguzi, uhuru wa vyombo vya habari, haki ya mikutano ya kisiasa na ulinzi wa mawakala wa vyama siku ya uchaguzi.
Suala linguine linalotajwa kuchochea kile kinachoitwa maandamano ya Oktoba, ni matukio ya utekaji yanayodaiwa kuripotiwa kwa wingi hivi karibuni hasa kwa wanaharakati na wapinzani wa Serikali. Hata hivyo Serikali imekanusha mara kadhaa kuhusika na matukio hayo, huku jeshi la Polisi likisema wapo wanaojiteka na kwamba linafuatilia kila taarifa na kuzifanyia kazi.
Historia ya maandamano nchini
Chanzo cha picha, AP
Tanzania ina historia ya muda mrefu ya maandamano ya kisiasa. Tukio linalokumbukwa zaidi ni maandamano ya Zanzibar ya Januari 27, 2001, yaliyopinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000. Watu 35 waliripotiwa kuuawa, zaidi ya 600 kujeruhiwa na maelfu kukimbilia nchi jirani, kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch.
Kwa upande wa Tanzania Bara, katika kipindi cha miaka 2005 hadi 2015, maandamano mengi yaliongozwa na vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, kiasi cha kupachikwa jina la utani ‘Chama cha Maandamano’.
Lakini hali hiyo ilibadilika katika awamu ya tano, ambapo ukali wa vyombo vya usalama uliongezeka na maandamano mengi kuzimwa mapema.
Mwaka 2024, chama hicho kilijaribu kuandamana kupinga kile kilichodaiwa kuwa ukosefu wa uwazi katika utekaji wa wanachama wake. Hata hivyo, viongozi wake walikamatwa na polisi kabla ya maandamano kufika popote.Na yapo mengi kama haya ambayo yalitangazwa na hayakufanyika, kwa watu kutojitokeza ama kudhibitiwa na vyombo vya usalama.
“Sioni uwezekano wa hayo maandamano (kufanyika), shida ambayo tunayo hapa ya hayo maandamano, kusema watu waandamane kwa sababu ya No Reforms No election, ni kitu ambacho hukioni kikitokea, labda litokee tukio ambalo litanyanyua hasira za watu, kama hakuna issue inayogusa maisha ya mtu (hawawezi kuandamana) anasema mchambuzi wa siasa Tanzania, Ezekiel Kamwaga, alipozungumza na The Chanzo.
Mchambuzi wa siasa na jamii, Rehema Mema, anasema tofauti na zamani, harakati za sasa hazina nguvu ya kiitikadi.
“Maandamano yaliyopita yalibebwa na vyama vyenye misingi ya kisiasa na ufuasi mkubwa. Haya ya sasa ni ya kiraia zaidi, hayana nguvu ya kichama. Sioni yakifanikiwa sana, lakini bado yanaakisi hisia halisi za wananchi kuhusu mustakabali wa masuala mbalimbali,” anasema Mema na kuongeza licha ya kuwa na uwezekano mdogo wa kufanyika kwa mafanikio “hayapaswi kupuuzwa, hasa kwa kile kinachotokea duniani kwa sasa kuhuhu maandamano ya Gen-Z.”
Kauli ya Serikali- “Hakuna maandamano”
Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, Rais Samia Suluhu Hassan, anayewania muhula wa pili kupitia chama tawala CCM, amesisitiza kuwa Oktoba 29 itabaki kuwa siku ya kupiga kura tu.
“Ndugu zangu, tarehe 29 mwezi huu tutoke tupige kura. Mimi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Nasisitiza maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura, hakuna mengine,” amesema Rais Samia katika moja ya mikutano yake.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na viongozi wa dini, wakuu wa mikoa, na Jeshi la Polisi, wakisisitiza amani na utulivu wakati wa uchaguzi.
Kwa kauli hizi mustakabali wa siku ya Oktoba 29, unasalia mikononi mwa watanzania.
“Pande zote mbili, wapiga kura na wanaotaka kuandamana zinadai haki zao za kikatiba, na pande zote wanajiona wapo sahihi”, anasema Mema.
Lakini changamoto kubwa iko katika namna taifa litakavyoshughulikia kwa usawa haki hizo mbili bila kuvunja amani wala kudhoofisha misingi ya demokrasia. Hili linawagusa wananchi wa kawaida, wanasiasa na vyombo vya ulinzi vinavyosimamia masuala ya usalama.
Iwapo Oktoba 29 itakuwa siku ya amani na ushiriki wa kidemokrasia, au siku ya mgawanyiko na mvutano, itategemea busara za pande zote zikihusisha serikali, wanaharakati, wanasiasa, na wananchi katika kuheshimu misingi ya haki, mazungumzo na maridhiano.
Kwa mara nyingine, Tanzania iko kwenye jaribio la kuthibitisha kama misingi ya demokrasia inaweza kuhimili misukosuko ya tofauti za kisiasa, bila kuvunja amani na umoja uliodumu kwa zaidi ya nusu karne.