An injured man, in a brown shirt and black short, is carried on a stretcher

    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Africa
    • Author, Basillioh Rukanga
    • Nafasi,

Polisi katika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wamerusha mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani wanaoandamana kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Uchaguzi ulitarajiwa kuwa kunyang’anyiro kikali kati ya Rais Samia Suluhu na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ambaye ameshitakiwa kwa uhaini, mashtaka ambayo amekanusha na chama chake kususia uchaguzi huo.

Watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye maandamano katika baadhi ya miji ya Tanzania huku shughuli ya upigaji kura ukiendelea katika uchaguzi mkuu ambao umekumbwa na mvutano.

Waandamanaji waliwasha moto barabarani, kuharibu mabasi, na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye vituo vya mabasi ya mwendo kasi na miundombinu mingine ya umma.

Tumechoka… Tunataka Tume huru ya uchaguzi ili Watanzania wamchague kiongozi wanayemtaka, mmoja wa waandamanaji aliiambia BBC.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Chalamila alionya kuwa serikali itawachukulia hatua kali watu wanaovuruga amani katika jiji hilo.

Shirika la uangalizi wa mtandao NetBlocks limeripoti “kuvurugwa kwa muunganisho wa intaneti” katika taarifa kwenye mtandao wa X zamani Twitter.

Ripoti zinasema kuwa idadi ya wapiga kura jijini Dar es Salaam ilikuwa ndogo wakati vituo vya upigaji kura vi;opofunguliwa mapema Jumatano, huku wengi wakisita kujitokeza kwa kuhofia usalama.

Msemaji wa polisi alihakikishia umma kwamba hakuna tishio lolote kwa usalama wao, akisema “watu wanapaswa kujitokeza kupiga kura”, kulingana na ujumbe uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii.

Zaidi ya wapiga kura milioni 37 waliosajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa urais na ubunge.

Vyama 16 vidogo, ambavyo havina umaarufu, vimeruhusiwa kugombea urais dhidi ya Rais Samia, ambaye anawania muhula wa pili.

Mgombea pekee wa upinzani, Luhaga Mpina wa Chama cha ACT-Wazalendo, alienguliwa kutokana na taratibu za kisheria.

Rais Samia Suluhu Hassan mwenye vazi la rangi nyingi na vazi la kahawia akipiga kura

Chama tawala Chama Cha Mapinduzi CCM, kimetawala siasa za nchi kwa miongo kadhaa na hakijawahi kushindwa uchaguzi tangu taifa hilo lilipopata uhuru.

Kabla ya uchaguzi huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yalilaani ukandamizaji wa serikali, huku Amnesty International ikitaja “wimbi la ghasia” linalohusisha kutoweka kwa nguvu, mateso, na mauaji ya kiholela ya wanaharakati wa upinzani.

Serikali ilipinga madai hayo, huku maafisa wakisema kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Samia aliingia madarakani mwaka 2021 kama rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.

Hapo awali alisifiwa kwa kupunguza ukandamizaji wa kisiasa chini ya mtangulizi wake, lakini nafasi ya kisiasa tangu wakati huo imekuwa finyu, huku serikali yake ikishutumiwa kuwalenga wakosoaji kupitia kukamatwa na wimbi la utekaji nyara.

Tume ya uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokeo ndani ya siku tatu baada ya upigaji kura kukamilika.

Pia unaweza kusoma:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *