Uchumi wa Kenya umeendelea kusuasua ikilinganishwa na ule wa Tanzania katika eneo la Afrika Mashariki, hasa kutokana na utegemezi mkubwa wa mauzo ya bidhaa ghafi nje ya nchi jambo linalokwamisha ukuaji wa uchumi na kuongeza kiwango cha umaskini.

Hayo yamo katika Ripoti ya Ujumuishaji wa Bara la Afrika 2025 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU).

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla unafanya chini ya wastani wa bara katika juhudi za kuimarisha uchumi wake kupitia ubunifu, uongezaji thamani wa bidhaa na upanuzi wa sekta za uzalishaji.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, Kenya inajipata ikifanya vibaya zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku uchumi wake ukiendelea kutegemea zaidi mauzo ya bidhaa ghafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.

Kwa muujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Afrika, hali hiyo, imeathiri maendeleo ya viwanda na sekta ya uzalishaji nchini humo jambo linalochangia kupungua ajira, kipengele muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na umaskini.

Alama ya utofauti wa biashara katika EAC (0.3920) imebaki chini kidogo ya wastani wa bara la Afrika (0.4072).

Kwa upande wa utofauti wa biashara, Tanzania inaongoza kwa alama 0.4457, ikifuatiwa na Burundi, kisha Kenya.

Nchi zinazofanya vibaya zaidi ni Uganda (0.2848), Rwanda (0.2241) na Sudan Kusini (0.2116), hali inayoonyesha pengo kubwa kati ya wingi wa biashara na kiwango cha ubunifu wa uchumi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa biashara ya bidhaa za kati bado ni dhaifu, huku mitandao ya uzalishaji wa kikanda ikiwa haijakomaa ipasavyo.

Wataalamu wa Umoja wa Afrika wanapendekeza kuwa jumuiya ya Afrika mashariki EAC ichukue hatua maalumu za kupunguza pengo la biashara kwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ndani ya eneo, kukuza uzalishaji wa viwandani, na kuhamasisha uongezaji thamani wa bidhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *