Chanzo cha picha, Getty Images
Tunaangazia uchambuzi wa vyombo vya habari vya kimataifa tukianza na gazeti la The Guardian la Uingereza, ambalo linaangazia kile inachoeleza kuwa athari za “kujihusisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja” kwa Uingereza katika mzozo huo, kwa kutupia jicho zana za kijeshi zilizotengenezwa na Uingereza zilizopatikana katika maeneo ya vita.
Gazeti hilo linasema kwamba nyaraka zilizowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinaonyesha kugunduliwa kwa mifumo ya mafunzo ya silaha ndogo ndogo iliyotengenezwa Wales, pamoja na injini za Uingereza zinazotumiwa UAE, magari ya kivita yaliyopatikana na wachunguzi kutoka maeneo ya Rapid Support Forces huko Khartoum na Omdurman.
Gazeti la The Guardian linaeleza kuwa ushahidi huu unaibua maswali mapya kuhusu mauzo ya silaha za Uingereza kwa Umoja Falme za Kiarabu (UAE), ambayo inakabiliwa na shutuma za kusambaza silaha kwa vikosi vya waasi wa Rapid Support Forces licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa vya silaha kwa pande zote zinazozozana nchini Sudan.
Nyaraka zilizopatikana pia zinaonyesha kuwa serikali ya Uingereza iliendelea kutoa “leseni wazi” yaani” taarifa ya kisheria inayotoa ruhusa kwa umma kupata, kutumia tena, na kushirikisha kazi bila vizuizi” vya kusafirisha silaha hata baada ya Baraza la Usalama kuonya kwamba zinaweza kuelekezwa Sudan. Leseni hizi huruhusu mauzo ya nje bila vikwazo vikali kwenye eneo la mwisho.
Gazeti hilo lilinukuu wataalam wa ufuatiliaji wa biashara ya silaha wakisema kuwa sheria za Uingereza zinaitaka serikali kusitisha usafirishaji wowote wa silaha iwapo kuna “hatari ya wazi” kwamba silaha hizo zitatumika kufanya ukiukaji mkubwa. Walisema kwamba rekodi ya UAE ya kuhamisha silaha kwenye maeneo yenye mizozo kama vile Libya na Yemen ilipaswa kuwa ilichochea Uingereza kukagua leseni hizi mapema.
Mashirika ya Sudan nchini Uingereza yametaka uchunguzi huru ufanyike ili kubaini jinsi silaha hizo zilifika Sudan, na kuonya kuhusu “ushirikiano usio wa moja kwa moja” ambao unazidisha mateso ya raia.
Serikali ya Uingereza ililihakikishia gazeti hilo kwamba mfumo wake wa kudhibiti usafirishaji wa silaha ni “miongoni mwa mifumo mikali na ya uwazi zaidi duniani,” huku UAE ikikanusha tena kutoa msaada wowote wa kijeshi kwa vikosi vya Rapid Support Forces.
Huku majanga nchini Sudan yakiongezeka na mataifa yenye nguvu ya kimataifa kuhusika katika kuchochea mzozo huo, maswali kwa mara nyingine tena yanagonga vichwa ya watu: Je, ni kwa kiasi gani sera za Marekani katika miongo kadhaa zimechangia kuzuka au kuendelea kwa migogoro katika Mashariki ya Kati?
“Kuandika historia kwa kutatua migogoro kwa njia ya kijeshi”
Katika mapitio ya kitabu kipya kiitwacho “Kicking the Hornet’s Nest: U.S. Foreign Policy in the Middle East from Truman to Trump,” gazeti la The Washington Post linachunguza mwenendo wa sera za Marekani katika eneo hilo kwa zaidi ya miongo minane, na kueleza kuwa ni mfululizo wa maamuzi potofu ambayo yalikuwa na athari mbaya kwa vizazi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na Daniel Zogby wa Chuo Kikuu cha California, Berkeley, kinakosoa vikali mtazamo wa Washington kuhusu Mashariki ya Kati. Kinasema kuwa Marekani imekuwa ikitafuta mara kwa mara “kuandika histora kwa kutatua migogoro kwa njia ya kijeshi,” na kwamba kuegemea sana kwa nguvu za kijeshi kumesababisha matokeo yasiyo na tija, kuanzia kutambuliwa kwa Israel mwaka 1948, kupitia uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003, hadi kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia na Iran.
Mwandishi anaelekeza kwa kile anachokielezea kama “fursa zilizopotea” ambazo zingeweza kubadilisha mwelekeo wa eneo hilo, kama vile uwezekano wa kupatikana kwa amani kupitia mazungumzo nchini Palestina kufuatia Azimio la Mkutano Mkuu wa UN 181, au kupitisha sera tofauti ya kuzuia ambayo ingeweza kuzuia kuongezeka kwa mashirika yenye itikadi kali kama Al-Qaeda na ISIS.
Hata hivyo, pia anakosoa viongozi wa mitaa ambao walishindwa kutumia nyakati muhimu za kihistoria, akisisitiza kwamba mizizi ya migogoro ya eneo hilo sio ya Marekani pekee lakini pia inahusishwa na urithi wa ukoloni na mgawanyiko wa ndani.
Gazeti hilo linahitimisha mapitio yake kwa kuuliza swali la msingi: Je, Marekani ilihusika na machafuko katika Mashariki ya Kati, au haikuweza tu kutatua migogoro iliyopo? Inahitimisha kuwa kitabu hiki kinaitaka Marekani kufanya mapitio ya kina ya mkakati wake katika kanda na kuondoa fikra za “kutaka kuwa na mamlaka daima” hadi jukumu endelevu na la ufanisi zaidi la kidiplomasia na maendeleo.
Gazeti hilo linaongeza kuwa kuangaliwa upya kwa sera za Marekani hivi leo kunaingiliana na kuharakisha mabadiliko ya kidiplomasia huko Gaza, ambapo mataifa yenye nguvu ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Uturuki, yanajaribu kuwa na ushawishi huku kukiwa na pingamizi zinazoongezeka na ushindani.
Chanzo cha picha, Getty Images
Nini nafasi ya Uturuki huko Gaza?
Gazeti la New York Times liliangazia mpango wa Uturuki baada ya vita huko Gaza, na kufichua kwamba Ankara ilijitolea kusaidia Marekani kudhibiti hali ndani ya Ukanda huo baada ya kusitishwa kwa operesheni za kijeshi.
Usaidizi huu utajumuisha wa kiusalama na wa silaha kwa maeneo ambayo majeshi ya Israel yamejiondoa, pamoja na kuchangia katika ujenzi na kusimamia hali ya kibinadamu.
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anaona jukumu hilo kuwa ni fursa ya kuionyesha nchi yake kuwa nchi yenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo na kurejesha hadhi yake katika ulimwengu wa Kiislamu baada ya miaka mingi ya mvutano.
Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti hilo, Israel ilikataa ushiriki wowote wa Uturuki katika mipango inayokuja, ikizingatiwa kuwa Uturiki iko karibu kisiasa na Hamas na kwamba kuingilia kati kwake kunaweza kutatiza hali ya usalama.
Gazeti hilo limewanukuu maafisa wa Israel wakisema kuwa Uturuki “inajaribu kutumia vita hivyo kisiasa” na kwamba ushiriki wake katika hatua hii “haukubaliki.”
Gazeti la New York Times linaongeza kuwa Uturuki inafanya kazi kupitia njia za kimataifa na Kiarabu kujionyesha kama sehemu ya suluhisho, na sio kikwazo, kwa kutumia vizuri kasi ya kidiplomasia ambayo Washington imeipata kuhusu kubadilishana wafungwa na usitishaji mapigano kwa muda.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya miji mikuu ya nchi za Kiarabu inajikuta katika wakati mgumu kati ya kukaribisha mpango wa Uturuki na haja ya kuratibu na Marekani na Israel katika mipango ya baada ya vita.
Gazeti hilo linaamini kuwa mzozo kati ya Ankara na Tel Aviv unaakisi mapambano makubwa ya ushawishi katika Mashariki ya Kati.
Wakati Israel inataka kujumuisha usalama na uwepo wake wa kisiasa huko Gaza, Uturuki inajaribu kutumia eneo lake la kijiografia na ushawishi wa kisiasa kuwa sehemu ya ulinganisho baada ya vita katika eneo hilo.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi