S

Watanzania wanapiga kura leo
katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Rais Samia
Suluhu Hassan wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) anatazamiwa kutetea
nafasi yake kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Ni uchaguzi wa saba tangu
kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na unafanyika wakati vyama
vikuu vya upinzani vikiwa na misimamo tofauti kuhusu ushiriki wao katika
mchakato huu.

Chama kikuu cha upinzani,
CHADEMA, hakishiriki uchaguzi huo kikishinikiza mabadiliko ya mfumo wa
uchaguzi, wakidai unakipendelea chama tawala.

Wakati huo huo, chama cha
ACT-Wazalendo hakina mgombea urais baada ya Luhaga Mpina kuenguliwa na Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kutokidhi matakwa ya kikanuni.

Kwa mujibu wa INEC, vituo
vya kupigia kura vinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na vitafungwa saa 10:00 jioni
kabla ya kuanza kwa zoezi la kuhesabu kura mara moja baada ya upigaji kura
kukamilika.

Hapo jana, wakaazi wa visiwa
vya Zanzibar walipiga kura ya mapema kwa makundi maalum ikiwemo askari, maafisa
wa tume na wahudumu wa afya. Tume imesema maandalizi yote yamekamilika na
imewataka wapiga kura kufika vituoni mapema ili kuepuka msongamano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *