.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Lizzy Masinga
    • Nafasi, BBC Dar es Salaam

Mtandao pepe binafsi (au VPN) ni muunganisho salama kati ya kifaa chako na kompyuta nyingine kwenye mtandao.

Huduma za VPN ni muhimu kwa kufikia mifumo ya kompyuta yako ya kazini kwa usalama ukiwa mbali na ofisi. Lakini pia hutumiwa kwa kawaida kukwepa udhibiti wa serikali, au kuzuia kutambulika eneo mlengwa alipo na kuzuia kwenye tovuti za kupakulia filamu filamu.

Kwa mujibu wa mtandao wa teknolojia wa kaspersky, VPN hutoa fursa ya kuanzisha muunganisho wa mtandao unaolindwa unapotumia mitandao ya Umma.

VPN huwezesha kutumia mtandao kwa njia fiche na kuficha utambulisho wako mtandaoni. Hii inafanya iwe vigumu zaidi kwa washirika wengine kufuatilia shughuli zako mtandaoni na kuiba data.

Kwanini unahitaji kutumia huduma ya VPN?

Kurambaza kwenye wavuti au kufanya miamala kwenye mtandao wa Wi-Fi usio salama kunamaanisha kuwa unaweza kuwa unafichua maelezo yako ya faragha na tabia za kuvinjari.

Ndiyo maana VPN inapaswa kuwa ya lazima kwa mtu yeyote anayejali kuhusu usalama wao mtandaoni na faragha.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, umewahi kuingia katika akaunti yako ya benki mtandaoni kwenye ukumbi ukiwa kwenye hoteli kwa mfano ? Au labda umelipa bili ya kadi yako ya mkopo mtandaoni. Ikiwa umefanya hivi bila kuingia kwenye VPN kwanza, unaweza kuwa umefichua maelezo yako ya faragha na tabia za kurambaza kwa wadukuzi na wahalifu wa mtandaoni.

Isipokuwa tu kama umeingia katika mtandao wa faragha wa Wi-Fi ambao unahitaji nenosiri, vinginevyo data yoyote inayotumwa wakati wa vipindi vyako mtandaoni inaweza kuwa katika hatari ya kuchukuliwa na watu usiowajua wanaotumia mtandao sawa.

VPN huficha nini?

Kwa mujibu wa mtandao wa programu ya norton ya kupambana na virusi kuhakikisha usalama wa kompyuta,VPN inaweza kuficha habari nyingi ambazo zinaweza kuweka faragha yako hatarini. Mtandao huu umeeleza mambo matano VPN ina uwezo wa kuficha.

.

1.Historia yako ya kurambaza mtandaoni

Sio siri unapoenda kwenye mtandao. Mtoa huduma wako wa mtandao na anaweza kufuatilia karibu kila kitu unachofanya kwenye mtandao.

Tovuti nyingi unazotembelea pia zinaweza kuweka historia. Vivinjari vya wavuti vinaweza kufuatilia historia yako ya utafutaji na kuunganisha maelezo hayo na anuani yako ya IP.

Hapa kuna mifano miwili kwa nini unaweza kutaka kuweka historia yako ya kuvinjari kuwa ya faragha. Labda unaugua unatafuta mtandao kwa maelezo kuhusu matibabu. Bila VPN, unaweza kuwa umeweka wazi maelezo hayo kiotomatiki na unaweza kuanza kupokea matangazo yanayolenga ugonjwa ulio nao ambayo yanaweza kuvutia umakini zaidi.

2.Utambulisho wako na mahali ulipo

Mtu yeyote anayenasa anuani yako ya IP (utambulisho wa kifaa chako) anaweza kufikia kile ambacho umekuwa ukitafuta kwenye mtandao na mahali ulipopatikana ulipotafuta.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Fikiria anwani yako ya IP kama anuani ya kurejesha ambayo ungeweka kwenye barua. Inakuongoza kwenye kifaa chako. Kwa kuwa VPN hutumia anuani ya IP ambayo si yako mwenyewe, hukuruhusu kudumisha faragha yako ya mtandaoni na kutafuta mtandao bila kukutambulisha.

Pia umelindwa dhidi ya historia yako ya utafutaji kukusanywa, kutazamwa au kuuzwa. Kumbuka, historia yako ya utafutaji bado inaweza kutazamwa ikiwa unatumia kompyuta ya umma au iliyotolewa na mwajiri wako, shule au shirika jingine.

3.Eneo ulipo wakati wa kurambaza

Unaweza kulipia huduma za utiririshaji zinazokuwezesha kutazama mambo kama vile michezo ya kitaaluma.

Unaposafiri nje ya nchi, huduma huenda isipatikane. Kuna sababu nzuri za hili, ikiwa ni pamoja na masharti ya mikataba na kanuni katika nchi nyingine.

Hata hivyo, VPN itakuruhusu kuchagua anuani ya IP katika nchi yako.

Hiyo inaweza kukupa ufikiaji wa tukio lolote linalooneshwa kwenye huduma yako ya utiririshaji.

4.Kifaa chako

VPN inaweza kusaidia kulinda vifaa vyako, ikiwa ni pamoja na kompyuta ya mezani, kompyuta ya mkononi na simu dhidi ya kuchunguzwa.

Vifaa vyako vinaweza kuwa walengwa wakuu wa wahalifu wa mtandao unapofikia intaneti, hasa ikiwa uko kwenye mtandao wa umma wa Wi-Fi.

Kwa kifupi, VPN husaidia kulinda data unayotuma na kupokea kwenye vifaa vyako ili wavamizi wasiweze kutazama kila hatua yako.

5. Shughuli zako za mtandaoni – kudumisha uhuru wa mtandao

Kumbuka, VPN hulinda dhidi ya mtoa huduma wako wa mtandao kuona historia yako na kutazama namna unavyovinjari. Kwa hivyo umelindwa ikiwa wakala wa serikali atamtaka mtoa huduma wako wa mtandao kusambaza rekodi za shughuli zako za mtandaoni.

Ikizingatiwa kuwa mtoa huduma wako wa VPN hajaandika historia yako ya kuvinjari (baadhi ya watoa huduma za VPN huweka), VPN yako inaweza kusaidia kulinda uhuru wako wa mtandao.

VPN na matumizi ya sasa

Kwa mujibu wa GlobalWebIndex , idadi ya watumiaji wa VPN duniani kote iliongezeka zaidi ya mara nne kati ya mwaka 2016 na 2018.

Katika nchi kama vile Thailand, Indonesia na China, ambapo matumizi ya intaneti yalizuiwa na kuchunguzwa, mtumiaji mmoja kati ya watano wa mtandao hutumia VPN.

Nchini Marekani, Uingereza na Ujerumani, idadi ya watumiaji wa VPN iko chini karibu 5%, lakini inakua. Mojawapo ya vichocheo vikubwa vya utumiaji wa VPN katika miaka ya hivi karibuni limekuwa hitaji linaloongezeka la yaliyomo na vizuizi vya ufikiaji wa kijiografia.

Kwa mfano, huduma za kutiririsha video kama vile Netflix au YouTube hufanya video fulani kupatikana katika nchi fulani pekee. Ukiwa na VPN za kisasa, unaweza kutumia anuani yako kwa njia iliyojificha ili uonekane kuwa unavinjari kutoka nchi nyingine, kukuwezesha kufikia maudhui uyatakayo ukiwa popote.

Je, VPN ni salama?

Ni muhimu kutambua kwamba VPN hazifanyi kazi kama programu ya kina ya kupambana na virusi.

Ingawa zinalinda IP yako (utambulisho wako) na kuficha historia yako ya kurambaza, muunganisho wa VPN haulindi kompyuta yako dhidi ya kuingiliwa.

Ili kufanya hivyo, hakika unapaswa kutumia programu ya kuzuia virusi. Kwa sababu kutumia VPN peke yake hakukulindi dhidi ya Trojans, virusi, roboti au programu hasidi nyingine.

Mara tu programu ya kuharibu inapoingia kwenye kifaa chako, inaweza kuiba au kuharibu data yako, iwe unatumia VPN au la.

Kwa hiyo ni muhimu kwamba utumie VPN pamoja na programu ya kina ya kupambana na virusi ili kuhakikisha usalama wa juu wa kifaa chako.

VPN ni salama tu kama sera za matumizi na uhifadhi wa data za mtoaji wake. Kumbuka kwamba huduma ya VPN huhamisha data yako kwa seva zao na seva hizi huunganishwa kwenye mtandao kwa niaba yako.

Ikiwa watahifadhi kumbukumbu za data, hakikisha kwamba iko wazi ni kwa madhumuni gani kumbukumbu hizi zimehifadhiwa.

Watoa huduma wakubwa wa VPN kawaida huweka faragha yako kwanza kabisa. Kwa hivyo unapaswa kuchagua mtoa huduma unayemwamini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *