Kadri mgogoro wa kifedha unavyoendelea Marekani, watu milioni 42 wa nchi hii wanahofia kuhusu upatikanaji wa chakula chao.
Kwa kuendelea kwa mgogoro wa kifedha na kufikia wiki ya nne ya kufungwa kwa serikali ya shirikisho, watu karibu milioni 42 wa Marekani wanaotegemea misaada ya chakula sasa wana wasiwasi kuhusu iwapo watapata chakula au la.
Wakati Rais Donald Trump akiwa safarini nchini Asia, mgogoro wa bajeti katika mipango mikuu ya msaada wa chakula, SNAP (Programu ya Msaada wa Chakula kwa Watu Maskini) na WIC (Programu ya Chakula cha Wanawake, Watoto na Watoto Wachanga), umekaribia kuathiri mnyororo wa usambazaji wa chakula katika maduka na hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula kwa mamilioni ya Wamarekani masikini.
Wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chakula umekua mkubwa miongoni mwa raia wa Marekani wakati ambapo nchi hiyo inajivunia kuwa uchumi mkubwa zaidi duniani. Kufungwa kwa serikali ya shirikisho, tukio ambalo sasa limeingia wiki ya nne, si jambo la kisiasa tu, bali ni tishio halisi kwa maisha ya mamilioni ya raia wa Marekani; watu ambao huenda katika siku zijazo wakakosa chakula, ambacho ni hitaji lao la msingi. Programu za SNAP na WIC, ambazo ni nguzo kuu za usalama wa chakula kwa watu karibu milioni 42, zimekumbwa na ukosefu wa fedha na Idara ya Kilimo ya Marekani imetangaza kwamba kadi za manunuzi za elektroniki, ambazo watu hutumia kununua chakula cha kila siku, huenda zisichajiwe mwezi Novemba.
Mgogoro huu si jambo la ghafla; ni matokeo ya maamuzi ya kisiasa na mgawanyiko ambayo imesababishwa na viongozi wa Marekani. Kufungwa kwa Idara za serikali ya Marekani kutokana na kukosekana bajeti ni matokeo ya moja kwa moja ya mvutano kati ya Wademokrat na Warepublican, ambapo pande zote mbili hutumia mgogoro huu kama chombo cha shinikizo ili kufikia malengo yao. Wanapoata hasara na madhara katika mgogoro huo si wanasiasa bali ni watu wa kawaida.
Katika miaka ya hivi karibuni, kufungwa kwa serikali kumekuwa chombo cha mara kwa mara cha kupigania maslahi ya kisiasa, na kila mara, mamilioni ya raia wanakuwa mateka wa mazungumzo ya kisiasa katika Bunge na Ikulu. Warepublican wanajaribu kupunguza bajeti kwa kufunga mipango ya misaada ya kijamii, na kwa upande mwingine, Wademokrat wanadai hawaafiki sera hiyo ya utawala wa Trump.
Mgogoro huu unaonyesha kuwa kipaumbele cha wanasiasa si ustawi wa jamii bali ni kushikilia madaraka katika ajenda ya kisiasa na uchaguzi. Wakati chakula cha watu maskini kinageuzwa kuwa zana ya shinikizo la kisiasa, maana halisi ya demokrasia inajitokeza kuwa ni ya shaka; nchi inayojivunia kujiita mfano wa utawala wa watu, sasa imeonyesha kuwa ushindani wa kisiasa unathaminiwa zaidi kuliko haki ya watu kuishi. Kwa hakika, sasa usalama wa chakula kwa mamilioni ya raia wa Marekani umekuwa mateka wa mazungumzo ya kisiasa.

Hii ni licha ya kwamba viongozi wa Marekani kwa miaka mingi wamekuwa wakidai kuleta uhuru, ustawi, na fursa sawa kwa raia wao.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa kati ya Wamarekani nane, mmoja anahitaji msaada wa chakula. Hii inamaanisha kuwa umaskini Marekani ni sehemu ya jamii. Sasa, watu hao ambao hutegemea msaada ambao wenyewe ni mdogo kutoka kwa serikali ili kuishi, wanakabiliwa na njaa na utapiamlo wakiwa hawana pa kukimbilia.
Shinikizo la kufungwa kwa serikali haliathiri familia tu. Mnyororo wa usambazaji wa chakula kutoka kwa wazalishaji hadi maduka madogo pia uko hatarini. Shirikisho la Wauzaji wa Vitu vya Chakula la Marekani limeonya kuwa SNAP na WIC huchangia kiuchumi takriban dola bilioni 20 kila mwaka na kubunni nafasi za ajira 388,000. Ikiwa mpango huo utakatizwa, maduka madogo yatakuwa waathirika wa kwanza.
Greg Ferrara, Rais wa Shirikisho la Wauzaji wa Bidhaa za Chakula (NGA), amewasihi wabunge kutoka pande zote mbili kufikia makubaliano ili kufungua serikali. Alisema wauzaji wa chakula huru ni chanzo pekee cha bidhaa za chakula, maziwa, na vitu vingine vya virutubishi kwa familia nyingi, wastaafu, na wazee; hivyo kukatika kwa bajeti kumesababisha ugumu wa upatikanaji wa chakula kwa makundi haya.
Wakati huu, Idara ya Kilimo, ambayo inapaswa kuwa ngao na msaada, imechagua kukaa pembeni. Hata wakati ambapo wajumbe wa Kongresi walitoa ombi rasmi la kutumia hifadhi ya dharura kufadhili bajeti, Idara ya Kilimo ilisema haikuwa na mpango wa kufanya hivyo; uamuzi huu ni wa kujua na unamaanisha kuwa serikali ya Marekani imewatelekeza raia wake wakati huu wa mgogoro wa chakula.
Wakati wanasiasa huko Washington wakishughulikia migogoro ya kisiasa na biashara zao, familia nyingi kote Marekani zinajiuliza jinsi watakavyoweza kupata chakula kwa watoto wao mwezi ujao.
Mgawanyiko huu wa maumivu kati ya siasa na maisha halisi, unatoa picha wazi ya hali ambayo Marekani inakutana nayo leo: nchi yenye nguvu kwenye karatasi, lakini iliyo dhaifu katika hali halisi.
Nchi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikijipanga ina nguvu na uwezo mkubwa, sasa inatazama jinsi chuki na mgawanyiko wa kisiasa unavyopelekea raia wakose chakula.
Maamuzi ya kibinafsi na biashara za kisiasa zimevunjilia mbali usalama wa chakula na kulazimisha familia kusimama muda kwenye mistari mirefu ya vituo vya misaada ya chakula vinavyosimamiwa na na mashirika ya hisani. Mgogoro huu ni aibu kwa inayodaiwa kuwa tajiri huku mamilioni ya raia wake wakihofia jinsi watavyowalisha watoto wao.