Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia maandamano ya siku ya uchaguzi yaliyogeuka kuwa ya vurugu kufanyika jana, Jumatano, katika jiji hilo na maeneo mengine nchini Tanzania.

Kilichoanza kama wito wa kudai haki kimegeuka kuwa chanzo cha hasara kubwa kwa wafanyabiashara ambao sasa wanasema hawajui pa kuanzia.

Mfanyabiashara Paul Boniface, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, alieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kudhibiti huduma za intaneti kufuatia machafuko hayo, akisema hali hiyo imeathiri shughuli za biashara zinazotegemea mtandao.

“Natumia VPN kwa sababu intaneti imezimwa. Hili limeathiri sana mfumo wetu wa utendaji. Kwa sasa kazi zimesimama kabisa kutokana na ukosefu wa intaneti imara,” alisema Boniface.

Baadhi ya biashara za wasanii wa Tanzania pia zimeharibiwa na kuteketezwa usiku wa kuamkia leo.

Raia wa Tanzania wamelaumu wasanii walioonekana kumuunga mkono Rais Samiya wakieleza walifumbia macho yaliyokuwa yakiendelea nchini humo.

Vurugu hizo zimesababisha uharibifu wa mali ikiwemo kuvunjwa kwa vioo vya maduka, kuchomwa kwa sehemu ya ukuta wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mjini Arusha, pamoja na kuharibiwa kwa vituo vya mabasi ya mwendokasi, vituo vya kupigia kura, mabasi, na maeneo ya biashara.

Maeneo yaliyoathirika zaidina maandamano hayo ni Kimara, Magomeni, Ubungo, Kinondoni, Shekilango, na Tandale.

Vituo kadhaa vya polisi pia vimeripotiwa kushambuliwa katika purukushani hizo.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa nchini, huku hali ya kisiasa ikizidi kuwa na mvutano mkubwa baada ya kuondolewa kwa wapinzani kadhaa katika kinyang’anyiro cha urais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *