.

Uchaguzi nchini Tanzania umekumbwa na ghasia kufuatia maandamano yanayotaka kurekebishwa kwa sheria za uchaguzi nchini humo mbali na kupinga ukandamizaji wa wakosoaji wa serikali.

Watanzania hapo jana walishiriki katika Uchaguzi mkuu ili kumchagua rais wao, Wabunge na Madiwani.

Hii leo maandamano yameripotiwa kwa siku ya pili mfululizo katika miji kadhaa ikiwemo Dar es salaam , Dodoma, Mwanza na miji mingine ambapo Vijana waliojawa na hasira wameendelea kukabiliana na maafisa wa polisi.

Haya ndio tunayojua kufikia sasa :

Bunge la Ulaya latoa taarifa kuhusu uchaguzi wa Tanzania

Bunge la Ulaya limesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ‘hakuwa huru wala na haki .

Kulingana na taarifa ilioandikwa katika tovuti ya bunge hilo, shughuli hiyo ya kuwachagua viongozi nchini humo ilikumbwa na udanganyifu .

“Tunataka washirika wa kidemokrasia kusimama kidete kutetea demokrasia na haki za binadamu,” Taarifa hiyo ilisema.

Aidha bunge hilo limetoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema Tundu Lissu bila masharti.

Maandamano yazuka kwa siku ya pili mfululizo Tanzania

Polisi katika mji wa Dar nchini Tanzania wamefyatua risasi na vitoa machozi siku ya Alhamisi kutawanya waandamanaji waliorejea barabarani siku moja baada ya uchaguzi uliogubikwa na maandamano yenye vurugu, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Reuters.

Maandamano yalizuka mjini Dar es Salaam na miji mingine kadhaa wakati wa upigaji kura siku ya Jumatano, huku waandamanaji wakilalamikia kukamatwa kwa viongozi wakuu wa upinzani na kuzuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa Urais mbali na madai ya ukandamizaji wa wakosoaji wa serikali.

Kwa mujibu wa Reuters baadhi ya maeneo ambayo maandamano hayo yameripotiwa kufanyika hii leo ni pamoja na Mbagala, Gongo la Mboto and Kiluvya.

Serikali yawaagiza wafanyakazi wa umma kufanyia kazi nyumbani

Kufuatia kuzuka kwa maandamano hapo jana na mapema leo, Serikali ya Tanzania ilitoa taarifa ikitawaka watumishi wa umma kufanya kazi kutoka nyumbani hii leo tarehe 30 Oktoba 2025.

Msemaji wa serikali aliweka ujumbe katika mtandao wa Instagram akidai hatua hiyo inatokana na angalizo la usalama lililotolewa na jeshi la polisi.

Aidha taarifa hiyo imeongezea kwamba wananchi wasio na ulazima wa kutoka nje wameshauriwa kufanya shughuli zao nyumbani.

Wafanyabiashara wakadiria hasara Dar es Salaam

Wakati huohuo wafanyabiashara Jijini Dar es salaam wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia maandamano hayo yaliokumbwa na ghasia.

Kulingana na wafanyabiashara wa huduma za intaneti , hatua ya serikali kudhibiti mtandao imeathiri pakubwa shughuli zao.

Tume ya Uchaguzi Tanzania yaanza kutangaza matokeo

Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC imeanza kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

Hadi kufikia sasa ni mikoa minne pekee iliofanikiwa kuwasilisha matokeo yake.

Kulingana na matokeo hayo Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama tawala cha CCM Samia Suluhu Hassan anaongoza kulingana na kura zilizohesabiwa.

Mtandao waendelea kuminywa

Tanzania inaendelea kushuhudia siku ya pili ya kukatwa kwa mtandao hatua ambayo imefanya mawasiliano kuwa changamoto.

Hapo jana siku ya uchaguzi, shirika la kimataifa la uchunguzi wa mtandao wa Netblocks, lilisema kuwa limegundua kufinywa kwa mtandao kote nchini humo.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania watoa tahadhari ya kiusalama

Kulingana na tahadhari hiyo ubalozi huo umewataka raia wa taifa hilo kuepuka maandamano yanayoendelea, kuepekuka mikusanyiko ya watu kufuatialia kwa karibu taarifa za vyombo vya habari ili kujifahamisha yanayoendelea mbali na kuchukua tahadhari ya juu katika maeneo waliopo.

Hatua hiyo inajiri kufuatia maandamano yanayoendelea nchini humo.

Kulingana na taarifa hiyo kuna ripoti za maandamano kote nchini ambayo yamesababisha kuzuka kwa ghasia na kufungwa kwa baadhi ya barabara.

Ripoti hiyo imeelezea kwamba baadhi ya barabara kama ile ya kuelekea katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere imefungwa.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuhusu kuzimwa kwa mtandaohali ambayo imeathiri pakubwa mawasiliano.

Amri ya kutotoka nje

Mamlaka ya Tanzania hapo jana iliweka amri ya kutotoka nje katika jiji la Dar es Salaam, jiji kubwa la taifa hilo, kufuatia makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji siku ya uchaguzi.

Mkuu wa polisi wa Tanzania, Camelius Wambura, alitangaza kwamba amri ya kutotoka nje itaanza saa 18:00 kwa saa za huko na kuwataka watu kusalia majumbani. Hakusema ni lini vikwazo hivyo vitaondolewa.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Chalamila alitoa tahadhari kuwa serikali itawachukulia hatua kali watu wanaovuruga amani ya jiji hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *