 
Chanzo cha picha, Getty Images
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemtangaza Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais katika visiwa hivyo.
Dk. Mwinyi aligombea kwa tiketi ya chama tawala cha CCM, ambacho hakijawahi kushindwa uchaguzi tangu uhuru.
Zanzibar, eneo linalojitawala ndani ya Tanzania, lilipiga kura siku ya Jumatano.
Mwinyi, aliye na umri wa miaka 59, ameingia kwenye uchaguzi huu wa 2025 akibeba bendera ya CCM kwa mara ya pili mfululizo.
Je Mwinyi ni nani?
Safari yake kisiasa ilianzia mwaka 2000, alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mkuranga kwa upande wa Tanzania bara, na kisha mwaka 2005 kuhamia upande wa Zanzibar katika jimbo la Kwahani ambalo ameliongoza kwa miaka 15.
Katika kipindi chake cha miaka 20 ya ubunge amefanya kazi na marais watatu wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na rais wa sasa John Magufuli.
Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa naibu waziri wa afya na hayati Mkapa, katika miaka 10 ya Kikwete alipanda na kuwa waziri kamili na kuhudumu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Afya na Ulinzi.
Aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Ulinzi kwenye serikali ya Hayati Rais John Pombe Magufuli.
Ushawishi wa Mwinyi uliojengeka katika utumishi wake katika miongo miwili iloyopita ulijidhihirisha katika namna ambavyo alinyakua tiketi ya kuwania urais ya CCM.
Safari hiyo ilianza kwa zaidi ya wananchama 30 kuchukua fomu za kuwania, kisha majina matano yakapelekwa mbele ya vikao vya juu vya chama hicho kwa maamuzi. Katika kura za mwisho za uteuzi ndani ya chama, Mwinyi akipata kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote, mshindani aliyemkaribia zaidi alikuwa na kura 19.
Pamoja na uzoefu wake na ushawishi wake binafsi wa kisiasa, Mwinyi anatokea katika moja ya familia maarufu na kubwa kisisasa nchini Tanzania. Baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi ni rais mstaafu wa serikali za Tanzania na Zanzibar.
Kitaaluma, Mwinyi ni tabibu na amepata elimu yake nchini Tanzania, Misri, Uturuki na Uingereza.
Safari yake ya kuwania urais
Mwinyi, alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huu wa 2025 akibeba bendera ya CCM kwa mara ya pili mfululizo.
Kwa haiba, Mwinyi anatambulika kama kiongozi mpole na mtulivu, sifa alizopewa mara nyingi zikihusishwa na malezi yake ya kisiasa ndani ya familia yenye historia ya uongozi.
Amejijengea taswira ya kiongozi anayeamini katika utulivu na maelewano, mtindo unaofanana na ule wa baba yake, aliyewahi kuongoza Zanzibar mwaka 1984 na baadaye Tanzania kati ya mwaka 1985 na 1995.
Tangu kuingia madarakani, ameelekeza juhudi zake katika maeneo matatu makuu: utalii, uwekezaji na huduma za kijamii.
Pia amesifiwa kwa kuendesha Zanzibar yenye hali ya utulivu na mshikamano zaidi kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tofauti na misuguano ya kisiasa iliyoshuhudiwa kabla ya hapo.
