 
Chanzo cha picha, Getty Images
Siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuamuru kuanza tena kwa majaribio ya silaha za nyuklia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema anaamini kuwa hatua ya Bw. Trump ilionyesha kuwa “Marekani ndiyo mzalishaji hatari zaidi wa silaha za nyuklia duniani.”
Siku ya Alhamisi usiku, Oktoba 30, Bw. Araqchi aliandika kwenye Mtandao wa X (zamani Twitter): “Kwa kubadilisha jina la Wizara yake ya Ulinzi kuwa Wizara ya Vita, mnyanyasaji mwenye silaha za nyuklia anaanza tena majaribio yake ya silaha za nyuklia.”
Juzi, Jumatano, kabla ya mkutano na Rais wa China Xi Jinping, Donald Trump alisema kuwa amemuamuru Katibu wake wa Vita kuanza tena majaribio ya nyuklia ili kusawazisha nguvu za nchi kama vile Urusi na Uchina.
Marekani imesimamisha majaribio hayo kwa zaidi ya miaka 30.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia aliandika: “Muonevu huyu huyu anaufanya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran uonekane kuwa hatari na unatishia kufanya mashambulizi zaidi kwenye vituo vya nyuklia chini ya ulinzi wetu. Vitendo hivi vyote viko wazi .
Iran siku zote imekuwa ikikanusha kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa kijeshi na kusema kuwa ikiwa mwanachama wa NPT, Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, inapaswa kuwa na haki ya kuendelea kurutubisha uranium na mpango wake wa nyuklia chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Lakini Marekani, Israel, na nchi kadhaa za Ulaya kama vile Uingereza, Ujerumani, na Ufaransa zinadai kusitishwa kwa mpango wa nyuklia na ufikiaji kamili wa wakaguzi wa IAEA kwenye vituo vyote vya nyuklia vya Iran.
Bwana Araghchi alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kujibu kwa kupinga uamuzi huo wa Rais wa Marekani, akiandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Tangazo la kuanza tena majaribio ya nyuklia ni kitendo cha kurudi nyuma na kisichowajibika na ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”
Marekani ina silaha nyingi za nyuklia kuliko nchi nyingine yoyote duniani; Urusi iko katika nafasi ya pili na China ni ya tatu.
Marekani haijafanya majaribio yoyote ya nyuklia tangu 1992.
Agizo hilo lilijiri siku chache baada ya Bw Trump kulaani Urusi kwa kufanya majaribio ya kombora la nyuklia lenye masafa “yasio na kikomo”.
Katika chapisho lake la Jumatano jioni, Oktoba 29/Februari 29, rais wa Marekani aliandika kwamba “hakuwa na chaguo ila kuboresha silaha za Marekani wakati wa muhula wake wa kwanza,” akikubali “nguvu kubwa ya uharibifu” ya silaha za nyuklia.
Pia aliongeza kuwa mpango wa nyuklia wa China “utalinganishwa na ule wa Marekani ndani ya miaka mitano ijayo.”
Bw Trump hakutoa maelezo kuhusu jinsi majaribio hayo yangefanywa, lakini aliandika kwamba “mchakato huo utaanza mara moja”.
Uamuzi huo ni mabadiliko ya wazi katika sera ya muda mrefu ya Marekani.
Jaribio la mwisho la nyuklia la Marekani lilifanyika Septemba 23, 1992, kabla tu ya Rais wa Republican George H. W. Bush kusitisha majaribio Vita Baridi vilipoisha.
