.

Tarehe 29 Oktoba, 2025, raia wa Tanzania walipiga kura kuchagua kupata wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Ubunge, Uwakilishi na Udiwani. Zoezi hili liliendeshwa nchini kote.

Lakini kwa mara ya kwanza kabisa maandamano yakashuhudiwa siku ya uchaguzi katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo ambayo ilisifika kama kisiwa cha amani Afrika.

Siku iliyofuata, nilipata fursa ya kuzungumza na Godwin Gonde, mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia ambaye kwanza alianza kwa kuelezea hali ilivyokuwa.

“Leo tumeamka hali ni shwari, tumefungiwa mitandao ya kijamii hakuna mawasiliano lakini pia uwepo wa watu wanaoendelea na shughuli zao umepungua, maduka yamefungwa,” Bw. Gonde alielezea hali ilivyokuwa.

Kile ambacho Watanzania waliamkia baada ya kushiriki katika uchaguzi ni kufungwa kwa mtandao hatua ambayo ilifanya iwe vigumu kuelewa kile kinachoendelea. Na vilevile, serikali ilitoa taarifa ya kuwataka wafanyakazi wa umma kufanyiakazi nyumbani.

“…Kesho tarehe 30 Oktoba 2025, watumishi wote wa umma nchini wafanyiekazi nyumbani isipokuwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vyao vya kazi kama ambavyo wataelekezwa na waajiri wao,” Msemaji wa serikali, Gerson Msigwa, aliweka ujumbe huo kwenye mtandao wake wa Instagram.

Vikosi vya usalama vilikuwa vinashuhudiwa mitaani vikishika doria na pengine baadhi ya raia walikuwa wanapitia hali ngeni kwao ambayo hawajawahi kuishuhudia siku za nyuma.

Kwa mandhari iliyojitokeza, unaweza kusema hali ilikuwa tofauti na vile wananchi walivyozowea katika chaguzi zilizopita.

Maandamano ya siku ya uchaguzi yana maanisha nini?

.

Kwa yule anayeifahamu Tanzania atakapokutana na taarifa hii kidogo itamshangaza na hata kuanza kufikiria mara mbili. Ni jambo ambalo haijawahi kutokea kwa nchi ambayo imejulikana kuwa tulivu hasa eneo la Afrika Mashariki.

“Ni doa kwa nchi na mfumo mzima kwa kuwa tungeweza kuzuia haya maandamano kama tungekubali kuzungumza,” amesema Bw. Gonde.

Huenda pengine maandamano hayo yameiingiza Tanzania kwenye historia ya nchi ambazo zimeshindwa kufanya uchaguzi wake kwa amani na wananchi wametumia njia hii kuwasilisha matakwa walio nayo kwa serikali yao.

Kimataifa, Tanzania ni nchi ambayo imejenga taswira ya ujamaa na kwa miaka mingi wananchi wamejitahidi kutoathirika kwa misingi ya kikabila, kidini, kitamaduni au kiyovyote kile.

Gonde anasema kuwa tofauti zao zimekuwa ni zenye kuzungumzika na hakuna hata siku moja walikubali ziwagawanye kama wananchi.

Tumefikaje hapa?

.

Lakini kwa jinsi hali ilivyo, Tanzania imefikaje hapa?

Sijui kama itakuwa sawa kusema siku ya nyani kufa miti yote huteleza. Tanzania ni nchi ambayo raia wake wamekuwa watiifu kwa kiasi kikubwa na kwa wengine kutokea kwa jambo kama hili ni kitu ambacho hakingeweza kufikirika. Lakini nini kimechangia kitumbua kuingia mchanga?

“Katika mfumo ambao tumeulea, wa kipindi kilichopita, watawala wamekuwa na sauti juu ya wapiga kura. Na kutaka kubadilisha kile ambacho kimezoeleka huenda ikawa ndio chanzo”, alisema Bw. Gonde.

Ukivuta picha ya jinsi hali ilivyo kwa bara la Afrika na dunia nzima kwa jumla, raia mpiga kura amekuwa akichukuliwa kama asiye na sauti, Na je, viongozi wanaokuja kuomba kura wanajihusisha na raia kwa namna gani?

“Katika mfumo ambao tumekuwa nao, viongozi wamekuwa wakitoa matamko makali, magumu na kuonyesha kwamba huyu mpiga kura hana nguvu. Hiki ndio kilichochochea hapa tulipofika sasa hivi,” alisema.

Kwa tathmini ya haraka haraka, ahadi ambazo wanasiasa hushindwa kuzitimiza pia ni miongoni mwa yale ambayo huingiza pabaya wanasiasa. Raia katika nchi kadhaa Afrika wamekuwa wakilalamikia hili. Na mwishowe, uhusiano wa mwanzo ambao uliowaunganisha na viongozi wao unaanza kudorora taratibu.

Vile vile, katika siku za hivi karibuni, nchi kadhaa zimekumbwa na maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na vijana maarufu kama ‘Gen Z’.

Kizazi hiki cha vijana ‘Generation Z’ kimekuwa kikitikisa tawala na kuibua mijadala kuhusu haki za kijamii, nafasi ya vijana katika siasa, na mustakabali wa uchumi.

Nchi za hivi karibuni kujikuta katika zahma hii ni pamoja na Madagascar, Peru, Nepal, Morocco na nyinginezo. Hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili kushuhudiwa. Miaka ya nyuma, nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini pia ziliathirika ambapo wananchi waliamua kuleta mwamko mpya hasa katika nchi za Kiarabu.

Tofauti na vizazi vilivyotangulia, Gen Z imekua katika mazingira ya kidijitali ambapo mitandao ya kijamii ni chombo cha uratibu na sauti ya pamoja kwao. Ni vigumu kujua ikiwa kwa namna moja au nyingine, hili limechangia kukatwa kwa mtandao nchini Tanzania.

“Sura ya maandamano yaliotokea Tanzania si ya vijana peke yake bali ni ya makundi mbalimbali. Yamegusa watu wa kata mbalimbali. Walio na mitandao ya kijamii na wasio nayo, wote wamejitokeza barabarani kutaka kuonyesha kutoridhika kwao na yale yanayoendelea,” Mchambuzi Gonde alisema.

Cha muhimu zaidi ni kwamba yamethibitiwa na usalama kuimarishwa. Lakini wengine bado wanajiuliza je, maandamano ya vijana yamekuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko ya kudumu? Hilo ni suali jingine tofauti kabisa ambalo nalo pia linahitaji kuchambuliwa kivyake.

Cha kujifunza kwa Afrika Mashariki

.

Kwa kuwa maandamano si jambo geni hasa nyakati hizi ambapo inageuka kuwa namna ya raia kuwasilisha ujumbe, Afrika Mashariki ina chochote cha kujifunza?

“Cha msingi zaidi ni kuheshimu matakwa ya watu kwa sababu watu ndio wenye serikali na wenye nchi na wanaoamua mustakabali wa maisha yao,” Gonde ameendelea kueleza.

Wakati umefika kwa Afrika kutambua kuwa mwananchi anahitaji aheshimiwe lakini pia awe na nguvu juu ya yule anayemchagua kwa sababu kiuhalisia, viongozi wanachanguliwa kumwakilisha mwananchi na huenda mambo yakanyooka kwa yule atakayekuwa na sikio la kuwakisiliza na kutenda.

Kuwa na weledi wa uongozi hakika sio jambo la kulala na kuamka labda kwa malaika, badala yake linahitaji hekima, busara na unyenyekevu.

Lakini pia, Bw.Gonde anasisitiza “tusiruhusu tofauti zetu wala itikadi zikatugawanya kwa sababu demokrasia ni mchakato mpana unaohitaji furaha ya wengi lakini kuridhishwa pia kwa wachache.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *