Chanzo cha picha, Reuters
Waandamanaji wameingia mitaani nchini Tanzania kwa siku ya tatu mfululizo, kukaidi amri iloyotolewa na mkuu wa jeshi la nchi hiyo ya kukomeshe vurugu hizo.
Maandamano yamekuwa yakifanyika katika katika miji mikuu waandamanaji wengi wao vijana wanaojulikana kwa jina maarufu kama Gen Z wakitaja uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano kutokuwa huru na wa haki kwa sababu viongozi wakuu wa upinzani walizuiliwa kugombea dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Bado mtandao wa intaneti umeminywa katika hatua ambayo imefanya kuwa vigumu kuthibitisha ripoti za mauaji huku mamlaka zikirefusha amri ya kutotoka nje katika juhudi za kudhibiti maandamano hayo.
Umoja wa Mataifa imeoa wito kwa vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji
“Tumetamaushwa idadi ya vifo na majeruhi yaliyoshuhudiwa katika maandamano yanayoendelea nchini Tanzania. Repoti tulizopokea zinaashiria kwamba watu takribani 10 wameuawa,” Shirika la habari la Reuters lilimnukuu msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu Seif Magango akisema.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Kenya limeiambia BBC kuwa mawasiliano yamekatizwa katika nchi jirani ya Tanzania na halijaweza kuthibitisha ripoti za vifo.
Hospitali nchini humo hazikubali kutoa taarifa kwa waandishi wa habari au mashirika ya kutetea haki za binadamu wanapoulizwa kuhusu visababishi.
Serikali imejaribu kupunguza kiwango cha vurugu.
Tume ya uchaguzi imetangaza matokeo kutoka takriban mikoa 80 kati ya mikoa 100 nchini, kituo cha utangazaji cha serikali TBC kinaonyesha.
Rais Samia anatarajiwa kushinda uchaguzi huo kwa tiketi ya Chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimetawala nchi tangu uhuru mwaka 1961.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa Jumamosi.
Kiongozi mkuu wa dini ya Kiislamu Tanzania – Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally – amewataka Waislamu kusali nyumbani swala ya Ijumaa huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa ghasia.
Siku ya Alhamisi, mkuu wa jeshi Jenerali Jacob John Mkunda aliwaamuru waandamanaji hao kuondoka barabarani, akisema wanajeshi watashirikiana na vyombo vingine vya usalama kudhibiti hali hiyo.
“Baadhi ya watu walikwenda mitaani tarehe 29 Oktoba na kufanya vitendo vya uhalifu. Hawa ni wahalifu na vitendo vya uhalifu vinapaswa kukomeshwa mara moja,” Jenerali Mkunda alisema kwenye Televisheni ya serikali, na kuongeza kuwa jeshi “limedhibiti hali hiyo”.
Lakini waandamanaji wameingia tena kwenye mitaa ya mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam.
Visiwani Zanzibar – ambako wananchi huchagua rais wao- Hussein Mwinyi wa chama tawala cha CCM, amabye alikuwa anagombea muhula wa pili , ameshinda uchaguzi huo kwa aslimia 80 ya kura.
Upinzani huko Zanzibar ulisema kumekuwa na “udanganyifu mkubwa”, shirika la habari la AP liliripoti.
Watalii katika visiwa hivyo pia wanaripotiwa kukwama katika uwanja wa ndege, na kuachwa na ndege kwa sababu ya maandamano, ambayo yanayoendelea Tanzania Bara.
Waandamanaji hao wanaishutumu serikali kwa kuhujumu demokrasia, kwani kiongozi mkuu wa upinzani yuko jela na kiongozi mwingine wa upinzani alienguliwa kwenye uchaguzi huo, na hivyo kuimarisha nafasi ya Samia kushinda.
Tundu Lissu ambaye ni kiongozi mkuu wa upinzani yuko jela baada ya kufunguliwa mshataka ya uhaini ambayo anayakanusha na chama chake kususia kura.
Mgombea mwingine, Luhaga Mpina wa Chama cha ACT-Wazalendo, alienguliwa kutokana na taratibu za kisheria.
Vyama vidogo 16 ambavyo havina uungwaji mkono mkubwa wa umma kihistoria, viliruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo.
Samia aliingia madarakani mwaka 2021 kama rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.
Hapo awali alisifiwa kwa kupunguza ukandamizaji wa kisiasa, lakini hali ya kisiasa tangu wakati huo imeendelea kuminywa, huku serikali yake ikishutumiwa kuwalenga wakosoaji kupitia wimbi la utekaji nyara.