
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, kwa mara nyingine tena amepinga hatua ya Marekani na Israel ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, akiitaja kuwa ni uongo mkubwa.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii wa X siku ya jana Jumapili, Araqchi ameashiria uthibitisho wa hivi karibuni wa mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, ambaye amesisitiza kwamba Iran haijawahi kujaribu kutengeneza silaha za nyuklia.
Matamshi ya Grossi yalitolewa katika hotuba yake Umoja wa Mataifa, ambapo alisema, “Wairani hawakuwahi wala hawajaribu kutengeneza silaha za nyuklia.
Araqchi pia ameangazia maoni yanayounga mkono Iran ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad Al Busaidi, ambaye amesisitiza kwamba “hakuna tishio la nyuklia kutoka upande wa Iran.”
“Mwenzangu wa Oman, Mhe. Al Busaidi, mpatanishi anayeaminika kati ya Iran na Marekani, amefafanua kwamba hakukuwahi kuwapo ’tishio la nyuklia’ la Iran,” amesema Araqchi.
Amesisitiza kwamba Iran haikudhoofisha diplomasia, akiongeza kuwa, “Wale walioharibu meza ya mazungumzo walifanya hivyo.”