Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa na kutangaza kwamba, bado inaheshimu na kushikamana na ahadi zake za kukabidhi kwa Israel miili ya mateka wa Kizayuni waliouliwa na utawala wa Kizayuni wakati wa mashambulizi yake ya miaka miwili kwenye Ukanda wa Ghaza.

Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa na Khalil Al-Hayya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Ghaza.

Amesisitiza kuwa, Hamas imeshikamana na vipengee vya makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza yaliyosainiwa Sharm El-Sheikh nchini Syria. Ametoa taarifa hiyo wakati wa mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan huko Istanbul jana Jumapili.

Taarifa hiyo imesema kwamba ahadi hiyo inahusu kutafuta na kukabidhi miili iliyobaki ya mateka wa Israel pamoja na kuendelea na hatua ambazo Hamas imekuwa ikizifanyia kazi kitaifa, kama vile kuundwa kamati huru ya kutawala Ukanda wa Ghaza na majukumu yanayohusiana na kamati hiyo, hasa hasa kusimamia kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Israel kwenye ukanda huo na kuondolewa mzingiro.

Wakati huo huo, Brigedi za Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, zimetangaza kwamba timu zake zilikuwa tayari kufanya operesheni za kuondoa miili ya mateka wa Kizayuni katika eneo linaloitwa “Mstari wa Njano” na kufanya zoezi hilo mfululizo bila ya kusita hadi mateka wote wa Kizayuni waliofukiwa kwenye vifusi vya eneo hilo watakapopatikana na kukabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni.

Brigedi za Izzuddin al Qassam pia zimewaomba wapatanishi na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kutoa vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kuendeshea operesheni hiyo kwa wakati mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *