Chanzo cha picha, Reuters
Ni siku ya tano sasa ambapo mtandao wa intaneti umeminywa nchini Tanzania. Na katika muda huo wote imekuwa vigumu kwa vyombo vya habari, mashirika ya kijamii na yale ya kutetea haki za kibinadamu na muhimu kabisa raia wa nchi hiyo walio ndani na nje ya nchi kupata taarifa sahihi na kamili kuhusu hali ya kiusalama nchini humo.
Vyombo vya habari kama vile BBC vimejitahidi kuwasiliana na watu waliomo ndani ya Tanzania wakiwemo maafisa wakuu serikalini kuhusu idadi kamili ya waathiriwa wa maandamano yaliyoshuhudiwa kati ya Jumatano na Ijumaa wiki jana.
Na japo mitandao iko chini, tumeweza kwuasiliana kwa njia ya simu na waliomo hasa katika mji wa Dar es Salaam, wengi ambao wameelezea kusikia au kushuhudia ghasia karibu na walipo kuwa.
Baadhi wameiambia BBC wamesikia milio ya risasia hasa katika siku mbili za kwanza ambapo maandamano hayo yalishika kasi.
Lakini katika siku chache zilizopita taarifa za idadi kubwa ya watu kufariki kwenye ghasia hizo zimejitokeza mitandaoni huku vyombo vya kimataifa kwa mfano AFP vikiripoti kuwa waliofariki ni mamia.
Huku wengi wakisubiri serikali kufungua mitandao nchini humo, taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa nchini Kenya – kuhusu yanayojiri Tanzania zimesemekana sio zote zenye ukweli.
Kwa mfano, siku tatu zilizopita kulikuwa na video ya watu wakikimbia kwenye angatua ya uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kuwashinda nguvu polisi.
Video hiyo ambayo ilitajwa kama hali mbaya ya kiusalama katika maandamano ya wiki hii, ilikuwa ni tukio la raia wa Tanzania kupokea mwili wa Rais John Pombe Magufuli uliokuwa unarejshwa nyumbani baada ya kifo chake mnamo 2021.
Huku hali ikiripotiwa kuwa tulivu mjini Dar es Salaam video zinazosemekana kuonyesha hali halisi ya majeruhi na uharibifu unaoshuhudiwa kule zinaanza kujitokeza kwenye mitandao ya kijamii hasa ya X, Instagran , TikTok na Telegram nchini Kenya .

Watalaamu wa masuala ya mitandao na usalama wameonya kwamba katika hali hii ya mitandao kufungwa nchini Tanzania kuna hatari ya kuwepo kwa upotoshaji wa taarifa na taarifa zisizo za ukweli ama uthibitisho.
Akizungumza kwenye mahojiano na BBC mtaalamu wa masuala ya usalama George Musalama alisema: ‘ Ni muhimu kwa serikali kurejesha mtandao wa inteneti kwa sababu hali hii inachangia pakubwa kuwepo kwa hali ngumu ya kiusalama nchini.
Kwa sababu hakuna njia ya watu kupata taarifa halisi kuna nafasi ya propaganda kusambaa na huenda ikawaweka wengi katika hali ya taharuki.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania Balozi Thabit amesema kwamba serikali ilichukuwa hatua hiyo ya kuminya mtandao wa intaneti ili kudhibiti hali ya kiusalama kutokana na ghasia zilizoshuhudiwa tangu Oktoba 29.
Mkuu wa jimbo la Dar es Salaam Albert Chalima akizungumza na vyombo vya Habari nchini Tanzania amewataka Watanzania kuamini na kufuatilia taarifa ambazo zinatolewa na vyombo vya Habari vya ndani ya nchi kuhusu hali ianyojiri nchini humo.