.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati hali ya utulivu ikishuhudiwa kurejea katika maeneo mengi ya Tanzania baada ya maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi wiki iliyopita, familia kadhaa zimeieleza BBC kuwa bado wana machungu na wasiwasi juu ya hali ya maisha na kutowaona wapendwa wao.

Mama mmoja ambae ametaka atambuliwe kama mama Kassim ameiambia BBC kwamba hajawaona vijana wake wawili tangu Jumatano wiki iliyopita, ambayo ilikuwa siku ya uchaguzi mkuu.

Mtoto wake mmoja yupo salama na ameshindwa kurudi nyumbani kwa kuwa hakuna usafiri lakini wa pili ndio hawana kabisa taarifa zake.

“Sijui yupo wapi, sijui amekamatwa, sijui amejeruhiwa, sijui amelazwa, sijui amekufa eeh Mungu msitiri mwanangu. Ana miaka 21 tu! Tunasikia watu wameuawa kwa wingi tunasali na kuomba asiwe mmoja wao,” Ameiambia BBC kwa uchungu.

Mama huyo mkaazi wa Tandale jijini Dar Es Salaam anasema kuwa kinachowavuruga kama familia ni kuwa hawampati kabisa Kassim kwenye simu na hawajui wapi pa kuanzia kumtafuta.

“Simu yake haiiti kabisa. Tunaambiwa namba haipatikani. Tumeanza kumtafuta hewani toka Jumatano saa 11 jioni tuliposikia kuna marufuku ya kutoka nje. Hatuna namna ya kwenda polisi ama hospitali kumtafuta… Kaka yake tulimpata, yeye baada ya vurugu kulipuka alikimbilia kwa mjomba yake na ameshindwa kurudi kwa kuwa hakuna usafiri na bodaboda zimekuwa ghali.”

Shida ya usafiri pia imewakumba wengi ambao wameshindwa kufika majumbani kutokana na umbali wa walipokwama na zilipo familia zao.

Mafuta yamepanda bei mara nne kwenye soko la magendo, vituo vya mafuta vimefungwa, na usafiri wa umma umesimama. Ni bodaboda wachache pekee wanaoendelea kufanya kazi, wakitoza bei kubwa. Ukosefu wa mafuta na usafiri unakwamisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kama chakula.

David Juma (si jina lake halisi) ameiambia BBC kuwa amekwama katika kitongoji cha Mwananyamala tangu Jumatano na ameshindwa kurudi nyumbani kwake Mbagala.

Juma anasema alipoona vituo vya kupiga kura vimefunguliwa na hakuna purukushani yeyote ile asubuhi ya Jumatano alienda katika shughuli zake za ufundi Mwananyamala akitumia usafiri wa mabasi ya Mwendokasi.

“Ile nafika tu Mwananyamala, nikaona mtandaoni BBC inaripoti maandamano yamelipuka Ubungo, baada ya muda mfupi tukasikia yamefika Manzese, wakati najipanga niondoke ghafla tukaanza kusikia milio ya mabomu ya machozi na risasi karibu yetu, kumbe maandamano yalikuwa yashafika Kinondoni na vituo vya mwendokasi na vile vya watu kupiga kura vikawa vinashambuliwa. Hapo nikajua siwezi kutoka sasa hivi. Nikajipa moyo kuwa nitaondoka jioni hali ikipoa,” amesema.

Juma anasema japo utulivu umerejea alipo na pia nyumbani kwake Mbagala, anashindwa kurudi nyumbani kwa kuwa hakuna usafiri na maisha yamekuwa magumu kwa familia yake kwa kuwa hana pesa wala akiba.

“Nilikuwa na elfu 10 ($4) kwenye simu, nimewatumia Ijumaa wamenunua chakula ambacho kimeisha jana Jumapili, sina pesa tena, watoto wangu wana njaa, natafuta mtu wa kunipa pesa ama kunikopesha. Sijui nitarudi lini nyumbani.”

Japo maduka yanafunguliwa mchana, si watu wote wenye pesa ama uwezo wa kununua mahitaji muhimu ikiwemo chakula. Maduka mengi yamefungwa, mengine yakiishiwa bidhaa.

Shuhuda mmoja katika eneo la Kibamba ameileza BBC kuwa duka lililopo nje ya nyumba yake limevunjwa usiku wa kuamkia Jumapili.

“Wameiba vyakula tu, mchele, sukari, mafuta ya kula, unga wa sembe na ngano. Hawakuchukua kitu kingine chochote, tayari watu wanakabiliwa na njaa.”

Ni siku ya sita sasa tangu huduma za intaneti nchini Tanzania zikatwe, hatua iliyoathiri upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hali ya kiusalama kufuatia maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa kati ya Jumatano na Ijumaa wiki iliyopita.

Vyanzo vya kidiplomasia, viongozi wa upinzani pamoja na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yamedai kwamba mamia ya watu wameuawa katika ghasia hizo.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Thabit Kombo aliiambia BBC kuwa serikali haiwezi kuthibitisha idadi hiyo rasmi. Wengine wanasemekana kukamatwa au hawajulikani walipo, huku mashuhuda walioko Dar es Salaam wakieleza kusikia milio ya risasi katika siku mbili za mwanzo za maandamano.

Katika baadhi ya mitaa ya Dar Es Salaam watu wameanza kutoka nje ya nyumba zao na doria za polisi zinaonekana kupungua – hata hivyo bado maafisa wa usalama wapo katika barabara kuu. Aidha katika baadhi ya misikiti, watu wameanza kurejea kuswali tangu Jumamosi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *