.

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 ulishindwa kukidhi viwango vya kidemokrasia vya jumuiya hiyo, kutokana na vitisho vya viongozi wa upinzani, vikwazo vya uhuru na ukosefu wa uwazi wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Katika taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari, shirika hilo limesema ingawa siku ya upigaji kura kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya amani, “katika maeneo mengi, wapiga kura hawakuweza kueleza kwa uhuru mapenzi yao ya kidemokrasia.”

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa uchaguzi huo “ulipungukiwa na matakwa ya Kanuni na Miongozo ya SADC ya Kusimamia Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021)”, kigezo cha uchaguzi huru, wa haki, na wa kuaminika miongoni mwa nchi wanachama.

Ujumbe huo vilevile uliripoti kuhusu kutengwa kwa wagombea wa upinzani kwa kukamatwa, na kupewa vitisho – ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu kwa tuhuma za uhaini.

SADC imesema vitendo hivi vinadhoofisha demokrasia ya vyama vingi vya Tanzania na kukatisha tamaa ushiriki wa wapiga kura.

“Hatua kama hizo ziliunda uwanja usio sawa na kupunguza uwezo wa wapiga kura kufanya chaguo la kweli,” taarifa hiyo ilisoma.

Kuhusu matangazo ya vyombo vya habari, SADC imesema kwamba, vyombo vinavyomilikiwa na serikali vilipendelea chama tawala, wakati vyombo vya habari vya kibinafsi vilijishughulisha na kujidhibiti kwa sababu ya kuogopa kuchukuliwa hatua baada ya uchaguzi.

Ujumbe huo uliitaka serikali kutekeleza mageuzi ya kina, ikiwa ni pamoja na kuruhusu wagombea binafsi, kuwezesha mahakama kupitia matokeo ya uchaguzi wa urais, kuhakikisha ulinzi wa waangalizi wa uchaguzi, na kuwashirikisha vijana katika siasa.

“Kwa kuzingatia maoni ya Tume, na kwa kuzingatia hali ya awali ya taarifa hii, ni hitimisho la kijadi la SADC kwamba Uchaguzi Mkuu wa 2025 nchini Tanzania haukukidhi viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia,” iliongezea taarifa hiyo.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi Mwanachama mwanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Waangalizi waliokuwepo kutoka Afrika ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wengineo kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Hatahivyo saa chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kula kiapo alishukuru makundi hayo kwa maoni yao lakini akaweka wazi kuwa sio kila jambo walilotaka linaweza kutekelezwa ila Tanzania yenyewe ndio yenye uwezo wa kuamua nini cha kufanya na kunukuu maneno ya Rais wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa wakati akiapishwa kuwa rais mwaka 2000.

“Nawashukuru waangalizi wetu wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifu tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu mkubwa. Tumesikia pia waliodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi wenyewe tumeyaona. Maagizo ya kutuelekeza nini cha kufanya tumeyakataa,” mwisho wa nukuu ya Rais Benjamin Mkapa.

Rais Samia aliongeza kuwa hakuna aliyemkamilifu duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *