Katika kile kinachotafsiriwa kama harakati ya kibeberu na ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, Rais wa Marekani Donald Trump ameashiria kuwa siku za Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kuweko madarakani zinakaribia ukingoni, huku mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiwa unaongezeka sambamba na Washington kushamirisha kuwepo kwake kijeshi katika eneo la Carribean.

Katika mahojiano na kipindi cha Dakika 60 cha CBS News kilichorushwa hewani siku ya Jumapili, Trump aliulizwa na mtangazaji Norah O’Donnell kama siku za Maduro kama rais zinakaribia ukingoni, naye akajibu kwa kusema: “ninaweza kusema, ndiyo. Ninafikiri hivyo”. Pamoja na hayo rais huyo wa Marekani alifuta uwezekano wa kuanzisha vita rasmi dhidi ya Venezuela.

Hata hivyo, Trump alikataa kusema kama suala la uwezekano wa kufanya mashambulio ya ardhini ndani ya ardhi ya Venezuela lina ukweli au la.

“Nisingependelea kusema kwamba ningefanya hivyo,” alijibu kiongozi huyo bila kutoa maelezo zaidi.

Siku ya Ijumaa, rais wa Marekani alikanusha pia ripoti za vyombo vya habari kwamba kuna uwezekano mkubwa wa nchi hiyo kushambulia vituo na mitambo ya kijeshi ndani ya Venezuela na akawaeleza waandishi wa habari kwamba bado hajachukua uamuzi juu ya suala hilo.

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti kuwa serikali ya Trump imeamua kufanya mashambulio dhidi ya vituo vya kijeshi nchini Venezuela kama sehemu ya vita vyake vinavyodaiwakuwa ni dhidi ya “ugaidi wa madawa ya kulevya” na kwamba mashambulizi hayo yanaweza kutokea wakati wowote ule kutoka sasa.

Washington inamtuhumu Rais wa Venezuela kwamba anaongoza kundi la wahalifu la Cartel de los Soles, lenye makao yake makuu katika nchi hiyo ya Amerika Kusini. 

Tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Septemba, Marekani imefanya mashambulizi yasiyopungua 14, mengi zaidi katika Bahari ya Carribean na Pasifiki Mashariki, na kuua zaidi ya watu 64.

Taasisi za kutetea haki za binadamu na wataalamu wa sheria wamehoji na kukosoa uhalali wa operesheni hizo za kijeshi, wakisema kwamba mashambulizi ya Marekani kwenye boti zinazodaiwa kubeba mihadarati yanakiuka sheria za kimataifa.

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema, mashambulizi hayo “hayakubaliki” na akahimiza kufanyika uchunguzi huru juu ya kile ambacho ofisi yake imekielezea kama mauaji ya kiholela.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameishutumu Washington kwa kubuni vita dhidi ya nchi yake na kuyaelezea madai inayotoa Marekani kuwa ni “uchafu” na “uongo mtupu”.

Maduro amesisitiza kuwa, Venezuela “haizalishi majani ya kokeini” na akasema, harakati za kijeshi za Marekani karibu na pwani ya nchi yake zinaashiria kuanzishwa kwa “vita vipya na vya milele”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *