Chanzo cha picha, ICC
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeonya kwamba ukatili unaoripotiwa mjini El-Fasher unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa za mauaji ya halaiki, ubakaji, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nchini Sudan.
Wakati huo huo, serikali ya kijeshi ya Sudan inaendelea na mazungumzo kuhusu masuala ya usalama, kufuatia kutekwa kwa mji wa El-Fasher — ngome ya mwisho ya jeshi katika eneo la Darfur — na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).
Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, kiongozi wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, alikiri kwamba baadhi ya wanajeshi wake walihusika katika makosa na ameahidi kufanyia uchunguzi suala hilo.
Hemeti, ambaye alijipatia utajiri wake kupitia biashara ya ngamia na dhahabu, sasa ameibuka kama mtu mwenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa siasa za Sudan, huku wanamgambo wake wakidhibiti takriban nusu ya nchi.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva ameonya kwamba ukatili unaofanyika Al-Fasher unafikia kiwango cha mauaji ya kimbari, na amesema hali inayofanana na njaa kali inaendelea kutokana na hatua ya RSF kuzuilia misaada ya kibinadamu madai ambayo RSF wamekanusha.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kwamba “mji wa Fasher na maeneo yanayouzunguka huko Kaskazini mwa Darfur ndio kitovu cha mateso, njaa, ghasia, na uhamishaji wa watu.”
Amesisitiza pia kuwa kuna “taarifa endelevu za ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.”
Chanzo cha serikali ya Sudan kimeiambia shirika la habari la AFP kwamba mamlaka zinazingatia pendekezo la Marekani kuhusu kusitisha mapigano.
Washington, kupitia kundi la Quad, imekuwa ikisukuma juhudi za kusitisha vita na kuweka ramani ya amani ya kumaliza mzozo huo.
Kikundi cha Majadiliano ya Usalama cha Quadrilateral (Quad) ni jukwaa la kimkakati kati ya Marekani, India, Japani, na Australia, lililoanzishwa mwaka 2007.
Watu wasiopungua 40 nchini Sudan wameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga mazishi yaliyokuwa yakifanyika nje ya mji wa el-Obeid, ambao unashikiliwa na jeshi, katika jimbo la Kordofan Kaskazini, maafisa na wanaharakati wamesema.
Wamelilaumu jeshi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kwa shambulio hilo lililotokea Jumatatu katika kijiji cha al-Luweib, wakati waombolezaji walipokuwa wamekusanyika ndani ya hema. RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.
Mwisho wa mwezi Oktoba, kikosi cha RSF, ambacho kimekuwa katika vita na jeshi la Sudan kwa zaidi ya miaka miwili, kiliteka mji wa kimkakati wa Fasher baada ya mzingiro wa miezi 18.