SERIKALI imesema hali ya utalii na amani viko imara nchini Tanzania. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi alisema hayo alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani ulioanza jana jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Akichangia taarifa ya utekelezaji ya mwaka ya taasisi hiyo Dk Abbasi alisema Tanzania ni salama baada ya kadhia iliyojitokeza wakati wa uchaguzi. “Serikali imefanya jitihada na kurejesha nchi yetu katika hali ya utulivu na hivyo kuendelea kuwa salama kwa watalii na vivutio vyetu vyote mnavyovijua viko salama,” alisema. Aliongeza: “Nawakaribisha wajumbe wa Mkutano huu na wadau wengine wa utalii kuja na kuendelea kutembelea nchi hii ambayo ni kivutio bora Afrika kwa utalii wa safari”.

Aidha, mbali ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 32 pekee kati ya wanachama wa umoja huo wanaofikia 160 kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji leo pia Baraza Kuu hilo limeipitisha Tanzania kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuhakiki wanachama. SOMA: Wapinzani waguswa ahadi za Samia

Tanzania ilinufaika na programu mbalimbali ikiwemo kuandaa Mkutano wa Dunia Kanda ya Afrika wa Utalii wa Vyakula uliofanyika Arusha Aprili mwaka huu na kufadhiliwa baadhi ya programu za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya Safu za Milima ya Usambara. Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili matumizi ya akili unde katika kutangaza utalii na pia utachagua Katibu Mtendaji mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *