WATANZANIA wametakiwa kuitumia Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe mkoani Dodoma kupata ushauri ukiwemo wa kisaikolojia. Daktari katika hospitali hiyo iliyopo jijini hapa Godfrey Mkama alitoa ushauri huo baada ya klabu za mazoezi ya kukimbia za Dodoma kushiriki mazoezi na baadaye kufanya usafi katika hospitali hiyo.

“Mkaribie hapa kuna vitengo vya wataalamu wa saikolojia usisubiri uumwe, ukiangalia hivi sasa maisha yetu tunakimbizana hivyo kitu kidogo tuu utahitaji ushauri mfike hapa kuna wataalamu wa saikolojia watawahudumia kwa ufanisi,” alisema Dk Mkama.

Amewashauri wananchi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine kufika hapo na kupata huduma za matibabu zikiwemo za kibingwa ambazo zinatolewa na wataalamu bobevu waliopo katika hospitali hiyo. Pamoja na hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa ambao wanakabiliana na magonjwa ya akili, msongo wa mawazo, uraibu wa pombe, bangi na vilevi vingine, pia inatoa huduma nyingine kama za ushauri na kutibu magonjwa mengine.

Dk Mkama alisema, huduma za matibabu katika hospitali hiyo zimeboreshwa kutokana na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaatiba na vitendanishi katika hospitali hiyo. Pia, alipongeza kikundi hicho kufanya usafi katika majengo hayo kwani usafi huo uliofanyika katika majengo hayo pia unahamasisha jamii kushiriki mazoezi na kukabiliana magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya akili, kupunguza msongo wa mawazo pamoja na kuimarisha viungo vya mwili.

“Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa kwa kutupa vifaatiba vya kisasa na kuboresha miundombinu pamoja na kuongeza wataalamu ili wananchi wapate huduma bora za afya na uwekezaji uweze kuleta tija kwa jamii,” alisema Dk Mkama. SOMA: Huduma afya ya akili kuboreshwa

Hivyo akawashauri wananchi kuitumia hospitali hiyo kupata matibabu ya magonjwa mengine kutokana na uwepo wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, watoto, macho na mifupa ambayo ni nafuu kuliko hospitali nyingine nchini kwa kutumia bima au malipo taslimu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Bakar Abdulrahman alitoa rai kwa wanamichezo wote kutunza afya zao kwa kupunguza matumizi ya wanga pamoja na sukari na kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *