Watanzania wahimizwa kupenda nchi, kulinda amaniWatanzania wahimizwa kupenda nchi, kulinda amani

VIONGOZI wa dini na watu mbalimbali wametoa mwito kwa wananchi kuipenda nchi yao na kulinda amani kwa kuzingatia falsafa ya 4R.

Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel Maasa amesema ni muhimu kutekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya).

Askofu Maasa alilieleza HabariLEO falsafa hiyo ni tiba kwa yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.

“Si lazima yote yatakayoongelewa yakubaliwe, tunaweza kukubaliana katika kutokukubaliana kwa amani, tunahitaji diplomasia zaidi katika hili,” alisema.

Mwanasiasa mkongwe mkoani Arusha, Modesti Meikoki ameshauri Watanzania waipende nchi yao na rasilimali zake.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa diwani wa Kata ya Daraja Mbili na Naibu Meya wa Jiji la Arusha katika miaka ya 1985-1995 alisema si sahihi kufanya vurugu kwa kigezo cha maandamano na kwamba yaliyotokea yameleta simanzi kwa wananchi.

Mwananchi mkoani Kilimanjaro, Prosper Temba alisema ni muhimu serikali iweke mikakati ya kuwezesha wananchi kutambua umuhimu wa kuvumiliana ili kuwa na amani.

Katibu wa Baraka Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Kilimanjaro, Alhaj Awadh Lema alisema ni muhimu wananchi kufundishwa uzalendo.

“Kwa mfano NGOs nyingi zinafanya kazi kwa karibu na wananchi wengi walioko kwenye makundi mbalimbali; wakati wa kutekeleza majukumu yao, kuwe na semina maalumu ambazo watashirikiana na sisi viongozi wa kidini kwa ajili ya kutoa elimu ya uzalendo na umuhimu wa kulinda amani ya nchi,” alisema.

Imeandikwa na Veronica Mheta (Arusha), John Mhala (Arusha) na Heckton Chuwa (Moshi).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *