Korosho Marathon yaja kwa watoto, wazeeKorosho Marathon yaja kwa watoto, wazee

BODI ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Kampuni ya Rhino Sports Talents Promotion imezindua vifaa vya mbio za Korosho Marathon msimu wa nne, huku mwaka huu zikitarajiwa kuwahusisha pia watoto na wazee. Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Novemba 29, 2025 mkoani Mtwara, zikiwa na lengo la kutangaza fursa katika tasnia ya korosho, kuhamasisha ulaji wa korosho na kuongeza thamani ya zao hilo.

Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, Revelian Ngaiza, amesema mbali na mbio za kilomita 5, 10 na 21, mwaka huu kutakuwa na mbio maalumu za kilomita 2.5 kwa watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 13, na kilomita 3 kwa wazee wenye umri wa miaka 60 hadi 95. “Tunapanua wigo wa ushiriki ili kujenga kizazi kinachothamini afya na michezo, sambamba na kuimarisha uelewa kuhusu zao la korosho,” alisema Ngaiza.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amepongeza waandaaji wa mbio hizo na kuwataka wadau, wawekezaji na wazazi kujitokeza kushiriki, akisema ni fursa nzuri ya kuimarisha umoja na afya kwa jamii. “Ni jambo zuri kuona wazee na watoto wakihusishwa.

Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo kutoka Rhino Sports, Nelson Mrashan, amewataka wazazi kusajili watoto wao ili kuwajenga katika misingi ya riadha tangu utotoni. “Riadha inaanzia chini. Tunataka kupata wakimbiaji watakaofikia viwango vya kimataifa,” alisema Mrashan. SOMA: Geay atakiwa kuibeba Tanzania riadha Berlin

Msemaji wa mbio hizo, Mohammed Kemkem, amesema zaidi ya washiriki 3,000 wanatarajiwa kushiriki mwaka huu, na kabla ya mbio hizo kutakuwa na Maonyesho ya Korosho yatakayofanyika kuanzia Novemba 24 hadi 28, yakionyesha shughuli na bidhaa zinazohusiana na zao hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *