CCM yampongeza Rais Samia kusamehe vijanaCCM yampongeza Rais Samia kusamehe vijana

DODOMA: MWENYEKITI wa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Maganya Rajab amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta maridhiano na kusamehe vijana walioshiriki vurugu na kusisitiza kuwa, hatua hiyo si woga bali ni ukomavu wa uongozi.

Aliwasihi vijana wa Tanzania kuacha tabia ya kufuata mkumbo na kuhatarisha usalama wa nchi. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Rajab alisema hotuba ya Rais Samia inatoa ujumbe mzito wa kuonesha utayari wa serikali ya CCM kuleta maridhiano miongoni mwa Watanzania na ikielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza uzito wa makosa yaliyofanywa na watuhumiwa wa vurugu hizo na kuwasamehe.

“Sisi kama wazazi, tunapokea hatua hii kwa mtazamo chanya. Tunampongeza Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa hatua hii ambayo ameichukua kama mlezi, kuhakikisha anatibu taifa, hasa vijana wetu. “Nisisitize kwamba, hatua hii sio woga, bali ni ukomavu wa uongozi, alioonesha rais ili tuendelee kuwa wamoja,” alisema.

Aliongeza: “Niwaombe Watanzania wenzangu, tuendelee kuienzi amani, tuendelee kudumisha utulivu, tuendelee kuleta mshikamano miongoni mwetu na katika nchi yetu, kama ambavyo imekuwa tunu yetu sisi Watanzania, kiasi ambacho tumekuwa mfano Afrika na dunia nzima hadi kuitwa hiki ni kisiwa na amani.”

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 13, Rais Samia alieleza masikitiko yake kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, siku ya Uchaguzi Mkuu ambazo zilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Pia, rais alitangaza kuundwa kwa Tume ya kuchunguza vurugu za uchaguzi ili kubaini chanzo cha vurugu hizo na hatimaye kufikia mazungumzo ya kuleta maelewano na amani nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *