RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hatovumilia ugomvi wa viongozi katika wizara ukiwemo wa mawaziri na makatibu wakuu. Dk Mwinyi ametoa msimamo huo katika hafla ya kuwaapisha mawaziri katika Ikulu ya Zanzibar juzi. “Zipo wizara watendaji walikuwa wanagombana, waziri na katibu mkuu wanagombana hawapatani, waziri na naibu waziri.
Naibu waziri na katibu mkuu, jambo hili sitalivumia tena…mifano ipo, sitegemei haya yatatokea huko tunakokwenda,” alisema Dk Mwinyi. Amesema viongozi hao wanapogombana kazi haziendi kabisa kwa sababu yanakuwa ni malumbano wakati wote kile mwenzake anataka yeye anazuia, hivyo kukwamisha maendeleo.
“Hamna sababu ya kugombana katika wizara, kukiwa kuna tatizo tupo, makamu wa pili yupo, mimi nipo. Njoo uniambie ni nini kinasababisha mgombane. Kwa sababu ukigombana wewe, waziri na katibu mkuu mkigombana kazi haziendi,” alisema Dk Mwinyi.
Aidha, aliwaagiza viongozi hao wasimamie nidhamu ya matumizi ya fedha kisheria na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. SOMA: Othman asisitiza wananchi kudumisha amani

Amesema katika eneo ambalo serikali haijafanya vizuri ni eneo la nidhamu ya ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi ya mapato hayo na kuongeza kuwa kuna viongozi ni mashujaa wa kulalamikia posho kuwa ni ndogo wakati wenyewe hawafanyi vya kutosha katika kukusanya mawazo.
“Hii isiwe hivyo, ndio maana tunasisitiza kuwepo kwa mifumo ya ukusanyaji fedha, zipatikane ndio matumizi yawepo, huwezi kuwa na matumizi wakati makusanyo hakuna. Hili napenda kulisisitiza kuwa makusanyo yataendana na matumizi,” alisema Dk Mwinyi.
Amesema matumizi lazima yazingatie makusanyo na ameonya safari zisizo na tija. “Tukusanye kwanza halafu tutumie. Lakini matumizi yenyewe basi yawe ni matumizi yenye tija, sio safari za kila siku. Tunatumia fedha nyingi sana katika safari, tunatumia fedha nyingi sana katika mafuta ambayo mengi ya mafuta tunayotumia tayari watu wameshapewa fedha hizo kwenye mishahara yao,” alisema.
Ameongeza : “Safari na mafuta imekuwa ni maeneo mawili yanayochukua fedha nyingi sana za serikali. Watu wanataka kusafiri kila siku. Safari moja ya mtendaji mmoja Dola za Marekani 5,000 maana yake ni karibu Sh milioni 12 zipo safari zenye tija na zipo safari hazina tija, kama wewe huwezi kuamua ipi ina tija na ipi haina tija nitakuamulia mimi”.

Dk Mwinyi aliwataka mawaziri hao wabuni mbinu bora zaidi ya kuondoa changamoto na wasisubiri kukumbushwa na Ofisi ya Rais. Ameagiza mawaziri hao wasikae ofisini na badala yake waende kwa wananchi kuwasaidia kutatua changamoto. “Wananchi wanataka viongozi washuke chini ili kero zao ziweze kutatuliwa.
Wengi wetu huwa tunabaki kwenye ofisi. Jumbe nyingi zinazoingia zinataka mawaziri watoke ofisini na kwenda kwenye maeneo yao ya utekelezaji,” alisema. Dk Mwinyi. Amesema ameacha nafasi nne za mawaziri na ikiwezekana zingine zitakuwa na manaibu mawaziri ili kutimiza takwa la kikatiba la kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Dk Mwinyi alikieleza Chama cha ACT Wazalendo kione umuhimu wa kuiunganisha nchi na watu wake kwa kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.