DODOMA: UAMUZI wa Rais Samia Suluhu Hassan kusamehe vijana waliofuata mkumbo na kushiriki vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu ni hatua inayostahili pongezi za dhati.
Akizungumza juzi jijini Dodoma wakati akifungua Bunge la 13, Rais Samia alitangaza msamaha kwa vijana na kuviagiza vyombo vya sheria, hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwachuja na kuwaachia huru vijana hao.
Akizungumza kama Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia alisema, “Navielekeza vyombo vya sheria, hasa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana. Kwa wale waliofuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya makosa, wawafutie makosa yao.”
Akiwa kama mama aliyebeba dhamana ya taifa hili, Rais Samia pia aliongeza kuwakanya vijana kwa kusema, Nasi tunapenda kusema kuwa, uamuzi wa Rais Samia kuwasamahe vijana hawa ni hatua inayostahili pongezi za dhati, hasa kipindi hiki ambacho taifa lilihitaji sauti ya utulivu na hekima.
Rais Samia amechagua njia ya kuponya badala ya kuumiza, kujenga badala ya kubomoa na kusikiliza badala ya kupuuza. Kwetu ni uamuzi unaodhihirisha uongozi unaotanguliza ustawi wa wananchi na mustakabali wa taifa, kuliko nguvu ya mamlaka.
Tuna kila sababu ya kumshukuru rais kwa hatua hii, kwani ameonesha uongozi wa kiutu, unaotambua kuwa sehemu kubwa ya vijana walioshiriki maandamano hayo hawakuwa maadui wa nchi, bali watoto wa taifa ambao baadhi yao hawakuwa wakijitambua na kujikuta wameingia kwenye jambo ambalo kimsingi halikuwa na manufaa kwa yoyote.
Uamuzi huo wa Rais Samia unadhihirisha uelewa wake mpana kama mzazi na mama, hivyo kitendo cha kuwapa nafasi ya pili ni kukiri kuwa makosa ya ujana yanaweza kurekebishika na serikali bora ni ile inayowalea vijana wake, badala ya kuwahukumu bila kutafakari matokeo ya muda mrefu.
Sambamba na hilo, tunaamini msamaha huo unarejesha matumaini katika majadiliano ya kitaifa na maridhiano. Rais Samia ameonesha kuwa amani haijengwi kwa pingu, bali kwa maridhiano; si kwa nguvu, bali kwa hekima.
Rais amewajengea Watanzania imani kubwa na ishara kuwa Tanzania inaweza kusonga mbele bila kubeba mizigo ya visasi. Uamuzi huu wa Rais Samia uwe funzo kuwa serikali inaweza kusikiliza na ni funzo kwa viongozi wengine wote kuwa wananchi si maadui, bali ni washirika katika kujenga nchi iliyo bora.
Pia, tunaamini hatua ya Rais Samia kuunda Wizara ya Vijana na kuwa na mshauri wake Ikulu ni kuwapa vijana fursa kujieleza, kushiriki na kutimiza wajibu wao bila hofu, haki, uhuru na uwajibikaji.
Tunasema kwa ujumla, msamaha wa Rais Samia kwa vijana hao ni ushindi wa busara dhidi ya hasira, amani dhidi ya misuguano na matumaini dhidi ya kukata tamaa. Rais Samia ametupa funzo muhimu Watanzania wote kuwa wakati mwingine, nguvu kubwa ya kiongozi haitokani na uwezo wa kuadhibu, bali uwezo wa kusamehe
