Kila la heri wanafunzi Kidato cha NneKila la heri wanafunzi Kidato cha Nne

MITIHANI ya taifa ya kidato cha nne imeanza leo nchini ikiwa ni kilele cha safari ya miaka minne ya masomo kwa maelfu ya wanafunzi wa shule zote za sekondari za serikali na binafsi. Wakati wanafunzi hao wakianza mitihani yao leo katika maeneo mbalimbali nchini hali ya utulivu imetawala, maandalizi ya kutosha na hamasa kutoka kwa walimu, wazazi na serikali na jamii kwa ujumla.

Mitihani hii ni muhimu kwani ni kipimo cha umahiri wa watahiniwa kwa yale waliyojifunza kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na taifa linahitaji kizazi chenye maarifa, stadi na maadili. Matokeo mazuri ya mitihani ya mwaka huu kwa wanafunzi wote 595,816 waliosajiliwa yanaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa dira ya maendeleo ya miaka ijayo.

Ni mitihani inayochukuliwa kama nguzo ya kwanza ya uchujaji wa wanafunzi kuelekea masomo ya sekondari ya juu, ufundi na vyuo vya kati. Kwa wengi, matokeo ya mtihani huu ndiyo yanayoamua mustakabali wao wa kitaaluma na hata fursa za ajira katika maisha yao katika miaka ijayo.

Kila mwanafunzi anapaswa kuiona nafasi hii kama daraja muhimu. Tunaamini walimu wa shule zote wamewaandaa wanafunzi vizuri muda mrefu kupitia marudio ya masomo, mitihani ya majaribio, ushauri wa kisaikolojia na semina za jinsi ya kujibu maswali.

Hivyo hatuna shaka kama watayazingatia haya. Hadi jana taarifa ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ilituhakikishia kuwa kwa upande wao maandalizi yote kwa ajili ya mitihani hiyo yalikuwa tayari yamekamilika. SOMA: Watahiniwa kidato cha nne waongezeka 7.6%

“Kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu,” ilisema taarifa hiyo.

Hivyo basi ni watahiniwa tu ndio waliobaki kutimiza jukumu lao kwa kufanya mitihani yao kwa utulivu na umakini. Wito wangu kwa wanafunzi, wazazi, walimu na wasimamizi wa mitihani hiyo, kila mmoja awajibike ipasavyo kwenye jukumu lake ili kufanya mitihani ifanyike kwa urahisi na kuepusha changamoto zenye kuweka vikwazo kwenye hatua hii muhimu. Kwa mfano kwa utamaduni wa wazazi wengi, mitihani imeonekana kama tukio kubwa la kijamii.

Familia nyingi hufanya sala na dua kwa watoto wao. Wengine huenda mbali zaidi kwa hatua za kiulinzi na kiusalama kwa kuwasindikiza wanafunzi hao shuleni ili kuhakikisha wanafika salama. Kama ambavyo wazazi na walezi kuichukulia hatua hii kama jambo muhimu, basi vivyo hivyo wafanye wadau wengine wanaohusika kuhakikisha mitihani hii inafanyika na kukamilika kama inavyotarajiwa.

Wakati huu Watanzania wote tunasema kila la heri kwa wanafunzi wa kidato cha nne nchini. Mfanye mitihani yenu kwa bidii, jitihada na nidhamu, kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu ili mpate matokeo yatakayounda kizazi cha wasomi, wataalamu mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *