TANGA: WAKAZI wa Kijiji cha Mseko, Idd Mohamed (55) na Huruma Mlengule (35) wamehukumiwa kwenda jela miaka 25 kwa hatia ya kupatikana na nyara za serikali na kumiliki silaha, kinyume cha sheria.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Husna Mwiula alitoa hukumu hiyo juzi. Alisema mahakama iliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na watuhumiwa wote wawili kupatikana na hatia.
Akifafanua hukumu hiyo, alisema kuwa kifungo cha miaka 20 gerezani ni kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali na washitakiwa hao wamefungwa kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kumiliki silaha isivyo halali.
Awali, ilielezwa kuwa Januari 5, 2025 katika eneo la Msubugo, Kijiji cha Mseko, Kata ya Kipumbwi, washitakiwa walikamatwa na Polisi wakishirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa Saadani wakiwa na nyama ya Digidigi watatu yenye thamani ya Sh 2,214,810 pamoja na silaha aina ya gobole.
Mashitaka hayo yalifunguliwa katika Kituo cha Polisi Pangani siku hiyo hiyo na upelelezi ukaanza mara moja ambapo upelelezi ulikamilika Mei 20, 2025 na washitakiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Pangani na shauri lilipewa namba 372/2025 na kupelekwa mbele ya Hakimu Husna Mwiula.
Awali, washitakiwa hao walikana mashitaka yao baada ya kusomewa na shauri liliendelea kwa kusikilizwa mashahidi wa upande wa mashitaka.
