TRA yaahidi kulinda biasharaTRA yaahidi kulinda biashara

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itashirikiana na wafanyabiashara kulinda biashara ili ziendelee kukua. Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema hayo alipowatembelea wafanyabiashara katika soko la kimataifa la Kariakoo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Nimekuja kuona shughuli wanazofanya lakini pia kuwapa pole kwa changamoto zilizotokea, kuna baadhi hawajafungua biashara nimekuja kuona biashara zinaendeleaje na nimefurahi kuona biashara zinaendelea kama kawaida na nimethibitishiwa na niliozungumza nao wanauza kama kawaida na wateja wanakuja,” alisema Mwenda.

Aidha, alisema biashara wanazofanya ni kwa manufaa ya umma kwa kuwa wakiwa wanafanya shughuli zao wananchi wanafaidika na huduma, kodi inayopatikana, kwa wengine kufanya manunuzi. “Rais Samia Suluhu wakati anafanya kampeni alisema Tume ya Rais ya kurekebisha masuala ya kodi imekamilisha kazi na serikali ikishaundwa itatoa ripoti yake. SOMA: Wadau wa kodi wataka haki mizozo na TRA

Moja ya changamoto walizozungumzia ni masuala ya kisera, nimewathibitishia kwamba pindi ripoti itakapotoka TRA itashirikiana nao kuhakikisha yale mapendekezo ya kutatua changamoto za muda mrefu yanatekelezwa na kutatuliwa,” alisema Mwenda. Alisema wafanyabiashara ni washirika wao hivyo changamoto zenye uthibitisho zilizojitokeza watachukua hatua za kuleta unafuu kwao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi alisema wamefurahi Mwenda amekwenda kuwapa pole kwa athari zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi. “Pamoja na lile sekeseke eneo letu lilibaki salama na sasa biashara zimechangamka, zimerudi kawaida tunatarajia kukua kuelekea mwisho wa mwaka. Hasara ni kubwa mtandao ulizimwa hatukufanya kazi, hivyo biashara za mtandaoni zilishindikana,” alisema Mushi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *