BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema idadi ya watahiniwa wa kidato cha nne imeongezeka kwa asilimia 7.67 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana. Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mtihani huo unaoanza leo hadi Desemba 5, mwaka huu.

Profesa Mohamed alisema watahiniwa 595,816 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wanafunzi 569,914 ni wa shule na 25,902 ni wa kujitegemea, katika jumla ya shule za sekondari 5,868 na vituo 813. “Watahiniwa hawa 595,816 waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 266,028 sawa na asilimia 46.68, huku wasichana wakiwa 303,886 sawa na asilimia 53.32,” alisema.

Ameongeza : “Watahiniwa wa shule wenye mahitaji maalumu ni 1,128, wakiwemo 860 wenye uoni hafifu, 70 wasioona, 58 wenye uziwi, watano wenye ulemavu wa akili na 135 wenye ulemavu wa viungo.” Profesa Mohamed amesema  kwa watahiniwa wa kujitegemea, wavulana ni 10,862 sawa na asilimia 41.93 na wasichana 15,040 sawa na asilimia 58.07.

Amesema 56 kati ya hao wana mahitaji maalumu wakiwemo 49 wenye uoni hafifu na saba wasioona.Profesa Mohamed amesema  maandalizi yamekamilika ukiwemo usambazaji wa mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka muhimu katika halmashauri zote Tanzania na Zanzibar, pamoja na maandalizi mahususi kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu.

Amesema kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimetoa semina kwa wasimamizi wa mitihani na kuweka mikakati ya kuzuia mianya ya udanganyifu, sambamba na kuimarisha usalama wa vituo vya mtihani kwa kuzingatia mwongozo wa baraza. “Kwa wasimamizi wa mitihani, baraza limewataka kufanya kazi kwa umakini, uadilifu na weledi ili kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake.

Aidha, wazingatie utoaji wa huduma stahiki kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu, ikiwemo mitihani yenye maandishi ya nukta nundu ambayo maandishi yaliyokuzwa na kuongeza muda wa kujibu kwa mujibu wa mwongozo,” alisema Profesa Mohamed.

NECTA imeagiza watahiniwa wafanye mtihani kwa kuzingatia kanuni za mitihani na kuepuka udanganyifu. Profesa Mohamed alionya yeyote atakayebainika atafutiwa matokeo. Ametoa wito kwa wamiliki na wakuu wa shule kutoingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani, na kusisitiza kuwa baraza litafuta kituo chochote kitakachobainika kuhatarisha usalama wa mtihani.

Profesa Mohamed  ametoa pia wito kwa jamii kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu, ikiwemo kuzuia watu wasiostahili kuingia katika maeneo ya mitihani na kutoa taarifa za udanganyifu kwa baraza. SOMA: NECTA yatangaza matokeo mtihani Elimu ya Msingi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *