ARUSHA; Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, amesema serikali imejipanga vema kuhakikisha changamoto ya ajira kwa vijana, wanawake na makundi maalumu zinaondoka.
Amesema hayo leo jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya ukusanyaji taarifa za viwanda Mikoa ya Arusha na Manyara yaliyoshirikisha maofisa Tehama na maofisa wa viwanda na biashara.
Amesema hatua ya hivi sasa ni kubaini viwanda vinavyofanya kazi na visivyofanya kazi, ikiwemo fursa za uwekezaji kwa mikoa ya Arusha na Manyara, huku mikoa mingine ikiendelea na utafiti.
Amesema lengo la semina hiyo ni kutekeleza maagizo ya Rais Samia Hassan Suluhu ya kuona uchumi wa viwanda nchini unakua kwa kufanya utafiti .
Amsema wanafanyia kazi maelekezo hayo ili kuwezesha ajira, uwekezaji na wazawa kubaini fursa za kuanzisha viwanda na uwekezaji katika mikoa mbalimbali kupitia taarifa sahihi za viwanda
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa ,Mkumbukwa Mtambo amesema serikali imebainisha viwanda vikubwa na vya kati ,vidogo na vidogo sana 23,150 katika mikoa saba.
Amesema baada ya ukusanyaji wa taarifa za viwanda hivyo nchi nzima, serikali itaviweka katika mfumo wa kanzidata ambao ni Mfumo wa Utoaji wa Taarifa za Viwanda (NIIMS), ili kuwezesha wawekezaji wa nje na ndani kuwekeza ili kukuza uchumi.
